MGANGA wa kienyeji, mkazi wa Kijiji cha Kirungu mkoani Kigoma, Wilson
Ndaliheremo (30), amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya
Kinondoni akikabiliwa na tuhuma za kumbaka binti (jina tunalo) mwenye
umri wa miaka 19.
Mbele ya Hakimu Joyce Mushi, Wakili wa Serikali, Daisy Makakala,
alidai kwamba mtuhumiwa alitenda kosa hilo Desemba 29, mwaka jana maeneo
ya Kawe Ukwamani.
Katika maelezo ya hati ya mashtaka, wakili huyo alidai mtuhumiwa
alimwingilia msichana huyo bila ridhaa yake kisha kumsababishia maumivu
makali sehemu zake za siri.
Baada ya maelezo hayo, mtuhumiwa alikana kutenda kosa hilo.
Wakili alidai upelelezi wa shauri hilo unaendelea hivyo akaomba tarehe nyingine ya kutajwa.
Hata hivyo, Hakimu Mushi alisema kwa mujibu wa sheria shtaka hilo
linadhaminika, hivyo alimtaka mtuhumiwa kuwa na wadhamini wawili
walioajiriwa serikalini au katika taasisi inayotambulika kisheria, pia
watakaoweka saini ya maandishi ya Sh milioni tano kila mmoja.
Mahakama imeahirisha kesi hiyo hadi Januari 30, mwaka huu
itakapotajwa tena na mtuhumiwa alirejeshwa mahabusu kwa kushindwa
kutimiza masharti ya dhamana.