HATIMAYE Aliyechomwa Mkuki Mdomoni Areja Nyumbani

MKULIMA na mkazi wa kitongoji cha Upangwani , Kijiji cha Dodoma Isanga , Kata ya Masanze, wilaya ya Kilosa , mkoani Morogoro , Augustino Mtitu,(35),ameruhusiwa kutoka Hospitalini alikolazwa.

Madaktari wamesema kwamba kuruhusiwa kwa mgonjwa huyo kumetokana na yeye kupona kufuatia kufanyiwa upasuaji mkubwa mara baada ya kuchomwa mkuki mdomoni na kutokea shingoni. Mtitu , alichomwa mkuki na kutokea shingoni Desemba 25, mwaka jana na watu wa jamii ya wafugaji wa kimasai.

Tukio hilo lililotokea majira ya saa tano asubuhi mwaka jana wakati alipokuwa shambani kuzuia vurugu zilizokuwa zimetokea baada ya wafugaji wa jamii ya kimasai kulisha mifugo yao kwenye shamba la maharage na mahindi yaliyopo katika kijiji hicho.

Mganga mkuu wa mkoa wa Morogoro, Dk Frank Jacob , akizungumza na mwandishi wa habari hizi jana alisema kuwa Mtitu ambaye alilazwa wodi namba moja ya wagonjwa wa majeruhi wa ajali na nyinginezo katika hospitali hiyo tangu Desemba 25 mwaka jana aliruhusiwa kutoka hospitalini hapo kwenda nyumbani baada ya kupona jeraha lilolotokana na mkuki na kufanyiwa upasuaji mkubwa.

Hata hivyo, Dk Jacob alimshukuru Mungu na madaktari , wauguzi kuwezesha kufanikisha upasuaji wa mgonjwa huyo uliofanikisha kuondolewa kwa mkuki aliochomwa mdomoni na kutokea upande wa shingoni .

Kwa upande wake Mtitu, akizungumza kwa njia ya simu akiwa Kilosa , alimshukuru Mungu , madaktari , uongozi wa halmashauri ya wilaya ya Kilosa na wananchi wa kijiji hicho kwa kuwezesha kunusuru maisha yake baada ya kuchomwa mkuki mdomoni uliotokea shingoni na kuweza kupona.

Mtitu amekaa wodini siku nane a baada ya kuruhusiwa , sasa anakwenda nyumbani kuungana na familia , ndugu na jamaa katika kijiji chao cha Dodoma Isanga , Kata ya Masanze, wilayani Kilosa.

Naye ndugu wa Mtitu, Mwalongo Sanga, akizungumza kwa njia ya simu kutoka kijiji cha Dodoma Isanga , alisema ndugu yao alifika mjini Kilosa ambapo familia yake ilikuwa inaishi kwa muda baada ya Mtitu kulazwa Hospitali ya Rufaa ya Morogoro.

Watu 12 wanashikiliwa na Polisi na kati yao saba wameshafikishwa katika mahakama ya wilaya ya Kilosa kujibu mashitaka ya kumchoma mkuki mkulima huyo na kufanya ghasia.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad