Jumla ya tani 35,491 za chakula zinahitajika ili kukabiliana na hali ya upungufu wa chakula na lishe kati ya mwezi Februari na mwezi Aprili mwaka huu unaowakabili watu 1,186,028.
Taarifa hiyo ya serikali imetolewa bungeni leo na Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Dkt. Charles Tizeba wakati akitoa kauli ya serikali kuhusu hali ya upatikanaji wa chakula nchini huku akisisitiza kuwa hali ya upatikanaji wa chakula nchini bado ni wa kuridhisha pamoja na kuwa baadhi ya maeneo yenye upungufu wa chakula.
Tizeba amesema taarifa hiyo ni kwa mujibu wa matokeo ya tathmini ya serikali iliyobaini kupungufu huo katika halmashauri 55 nchi nzima.
Aidha amesema kuwa jumla ya watu 118,603 wasio na uwezo wa kupata chakula watahitaji tani 3,549 za chakula cha bei nafuu kwa haraka na tayari serikali imeanza kuchukua hatua za kushusha bei ili wananchi waweze kumudu bei zake.
Amesema kutokana na kuchelewa kwa mvua na mtawanyiko usioridhisha katika maeneo mengi nchini athari zinazotarajiwa kutokea ni pamoja na matarajio ya malengo ya uzalishaji wa mazao ya chakula huenda yasifikiwe, uzalishaji wa mbegu za mazao ya kilimo utapungua, uwezekano wa kuongezeka kwa bei za baadhi ya mazao ya chakula upo, kupungua kwa mapato yatokanayo na ushuru wa mazao kwa baadhi ya halmashauri.
Athari nyingine ni pamoja na kuongezeka kwa migogoro baina ya wakulima na wafugaji kutokana na uhaba wa malisho na maji na uwezekano wa kupungua kwa mapato yatokanayo na mazao ya kilimo yanayouzwa nje ya nchi, uwezekano wa kuwa na maeneo mengi yenye upungufu wa chakula na hivyo kuongezeka kwa kiwango cha utapia mlo.
Dkt.Tizeba amesema kuwa ili kukabiliana na athari za ukame tathmini imebainisha kuwa halmashauri za wilaya hizo 55 zinahitaji jumla ya tani 1,969 za mbegu bora za mahindi, mtama na mizizi inayokomaa kwa muda mfupi na kustahimili ukame na mbegu hizo zinahitajika ziwafikie mwezi Februari mwaka huu ili ziweze kupandwa katika msimu wa mwaka 2016 /2017 katika maeneo yanayoendelea kupata mvua wakati huu wa mwaka.