MKUU wa Wilaya ya Uyui mkoani Tabora, Gabriel Mnyele ameachia ngazi wadhifa huo kuanzia jana.
Mnyele, ambaye alikuwa wakili maarufu nchini kabla ya kuteuliwa kuwa mkuu wa wilaya, imeelezwa kuwa ameamua kujiuzulu kwa sababu binafsi.
Lakini, akizungumza kwa simu jana, Mnyele alisema kwamba, “Ukiteuliwa, mamlaka husika inatoa taarifa, na ukiondoka katika nafasi hiyo mamlaka inatoa taarifa. Kwa hiyo mtafuteni Msigwa (Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu). Lakini sisi tuko huku tunaendelea na kazi.”
Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri hakupatikana kuelezea kwa undani uamuzi huo, lakini gazeti hili limethibitishiwa na viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Uyui kwamba Mnyele amejiuzulu na aliwaeleza hayo jana alipopita kuwaaga.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Uyui, Said Ntahondi alisema kwamba anawatakia kila la heri katika majukumu yao ya kazi. Alisema kwamba licha ya yeye (DC Mnyele) kuondoka, anatambua kuwa mapambano juu ya maendeleo ya Uyui, yataimarika kwa watumishi wote wa halmashauri hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa yao, Mnyele alipita kila Idara za Halmashauri ya Wilaya hiyo kuaga akianzia na watumishi wa ofisi yake.
Taarifa za awali zinasema kuachia kwake ngazi ya ukuu wa wilaya imetokana na kutingwa na majukumu mengi binafsi aliyonayo, na kwamba imedaiwa kuwa mkuu huyo wa wilaya aliandika barua mwaka jana akiomba kujiuzulu nafasi hiyo, kwani ametingwa na majukumu mengine binafsi.
Taarifa zaidi zinasema baada ya kuandika barua ya kuutema ukuu wa wilaya, barua yake imejibiwa na amekubaliwa kuachia nafasi hiyo.
Mnyele alikuwa mmoja wa wakuu wa wilaya 139 walioteuliwa na Rais John Magufuli, Juni 26, 2016, ambao ilielezwa kuwa amezingatia mambo kadhaa, ikiwa ni pamoja na umri ambapo kwa wale ambao umri wao ni zaidi ya miaka 60 ameamua wastaafu.