MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi(CUF) Profesa Ibrahimu Lipumba
amewataka wananchi wa kata ya Isage kutomchagua kiongozi katika ngazi ya
udiwani kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kwa kuwa
wanaweza 'wakamuuza' kama walivyofanya kwa Dk Wilbroad Slaa kwenye
Uchaguzi Mkuu uliopita.
Ameyasema hayo jana katika mkutano wa hadhara wa kumnadi mgombe wa
chama hicho, Saidi Juma uliofanya ndani ya kata ya Isagehe Wilayani hapa
Mkoani Shinyanga.
Lipumba alisema Chadema ilipitisha Dk Slaa kuwa mgombea urais, lakini
Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Freeman Mbowe alimuuza kisha kumpatia
nafasi hiyo aliyekuwa Waziri Mkuu wa awamu ya nne, Edward Lowassa.
“Msichague viongozi wapiga dili kwani mkimchagua diwani anayetoka
Chadema naye anaweza kuuzwa kama Mwenyekiti wao wa Taifa, Freeman Mbowe
alivyomuuza Dk Slaa uchaguzi mkuu uliopita mkaanza kuhangaika kutafuta
maendeleo, chagueni kiongozi atakayesimamia rasilimali za wanaisagehe,”
amesema Lipumba.
Pamoja na mambo mengine, Lipumba alisema wananchi wanatakiwa kuchagua
kiongozi bora atakayetambua changamoto za wanaisagehe ikiwa ni pamoja
na kusimamia rasilimali za wananchi na kuongeza kuwa kufanya hivyo
itafanya kata hiyo kupata maendeleo ya haraka.
“Kama wananchi mtamchagua Diwani wenu kupitia chama cha CUF ,basi
nitatoa ushauri wa mara kwa mara juu ya kunyanyua uchumi wa kata hii ili
kuleta maendeleo ya haraka kwa wananchi… binafsi ni mtaalamu wa
kutafuta wafadhili bahati nzuri shule ya Isagehe ilijengwa na kanisa la
pentekoste Sweden hivyo naweza kuwaunganisha nao,” amesema.
Mgombe wa kiti hicho cha udiwani, Saidi Juma alisema atahakikisha
anatekeleza yale yote aliyosema wakati wa kampeni ikiwa ni pamoja na
kumshirikisha Profesa Lipumba katika kumshauri namna ya kuongoza kata na
kutafuta wafadhili ili kata ipate maendeleo ya haraka.