MAELFU ya wakazi jijini hapa(Mbeya), wamelazimika
kusitisha shughuli zao kwa zaidi ya saa tano kushuhudia tukio la aina yake
baada ya familia moja kuzika jeneza tupu na kulazimisha Jeshi la Polisi
kulifukua.
Akithibitisha tukio hilo jana, Kaimu
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Emmanuel Likula, alisema tukio hilo
lilitokea juzi saa 4.30 asubuhi Igoma ‘A’, kata ya Isanga.
Alisema Jeshi la Polisi la Mkoa
lilipokea taarifa kuwa maiti aliyekuwa azikwe kwenye makaburi ya zamani ya
Isanga alikutwa chumbani kwenye godoro na kulazimika kulifukua siku iliyofuata.
Alisema baada ya taarifa hiyo, polisi
walifuatilia na kubaini kuwa juzi saa moja asubuhi Jailo Kyando (36) mwosha
magari na mkewe Anna Elieza (32) wakazi wa Mtaa wa Igoma ‘A’ waliamka na kukuta
mtoto wao wa kwanza Haruni Kyando (9) akiwa amefariki dunia.
Alisema taarifa za awali zilidai kuwa
marehemu tangu utotoni alikuwa na matatizo ya kifafa
hali iliyosababisha aishi bila kusoma.
Kaimu Kamanda alisema kwa kifo hicho
taratibu za mazishi zilifanyika na saa sita
mchana jeneza lililoletwa msibani liliwekwa sebuleni kando ya mwili wa
marehemu uliokuwa umeviringishwa kwenye blanketi na kulazwa kwenye godoro.
Alisema baada ya maombi ya na Walokole wa
Bonde la Baraka, vijana walibeba jeneza hadi makaburini na kuzikwa.
Aliongeza kuwa waombolezaji waliporudi
nyumbani walitaharuki kuona mwili wa Haruni chumbani umelazwa eneo ulipokuwa
awali.
Kutokana na hali hiyo, taarifa
zilifikishwa Polisi, askari walifika na kuuchukua mwili wa marehemu na
kuhifadhi kwenye mochari ya hospitali ya rufaa ya Mbeya.
Polisi walikwenda makaburini kusimamia
ufukuaji kaburi kuanzia saa 4.30 asubuhi hadi saa tano asubuhi.
Baada ya kufukua Mwenyekiti wa Mtaa wa
Igoma ‘A’, Fred Mwaiswelo alifunua jeneza na kukuta likiwa tupu hali
iliyoashiria kuwa mwili haukuwekwa.
Polisi walibeba jeneza hilo na kwenda
nalo kwenye kituo kikuu cha Polisi kwa uchunguzi zaidi kabla ya kuwakabidhi
ndugu kuendelea na taratibu za mazishi kwa mara nyingine.
Hata hivyo, baadhi ya ndugu na majirani
wa mtaa huo walisema tukio hilo linaweza kuwa na sura mbili; hujuma za makusudi
au bahati mbaya ya kusahau mwili.
Walisema inaweza kuwa hujuma kutokana na
kawaida ya misiba kabla ya mazishi lazima ndugu kutoa heshima za mwisho, lakini
msiba huo haukuwa na utaratibu huo na baadhi ya ndugu hawakuhudhuria maziko.