Hivi Ndivyo Kesi ya Babu Tale Ilivyopigwa Kalenda,Ashindwa Kulipa Milioni 250 ..!!!


SHAURI la Mkurugenzi wa Kampuni ya Tiptop Connections, Hamis Taletale ‘Babu Tale’ limepangwa kusikilizwa kwa Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Albert Mashauri baada ya Msajili wa Mahakama hiyo, Projest Kahyoza kujitoa katika shauri hilo.

Babu Tale ambaye ni Meneja wa mwanamuziki wa kizazi kipya, Nassib Abdul ‘Diamond’, anatakiwa aieleze mahakama kwa nini asifungwe jela baada ya kushindwa kulipa Sh milioni 250.

Anatakiwa kujieleza kutokana na kushindwa kutii hukumu ya mahakama iliyomtaka amlipe Mhadhiri wa Dini ya Kiislamu, Shehe Hashimu Mbonde fedha hizo baada ya kuuza kanda za mahubiri yake bila ridhaa yake Msajili Mashauri ameanza kusikiliza shauri hilo kwa kuahirisha kesi hiyo hadi Februari 16 mwaka huu baada ya Wakili wa mdaiwa, Robert Mkoba kuomba kuahirishwa shauri hilo hadi tarehe nyingine kwa kuwa anasikiliza kesi nyingine kwa Jaji Eliezer Felesh.

Hata hivyo, Wakili wa mdai, Mwesigwa Muhingo aliieleza mahakama hiyo kuwa mawakili wa mshitakiwa wapo watano hivyo imekuwaje aje wakili ambaye anajua kwamba ana kesi nyingine ya kusikiliza kwa jaji mwingine. Pia alidai kuwa waliwapa mawakili hao barua siku tatu kabla ya shauri hilo kwa lengo la kujipanga waende na wadaiwa.

Kutokana na hali hiyo, Msajili Mashauri aliahirisha kesi hiyo hadi Februari 16 mwaka huu kwa ajili ya mdaiwa kueleza kwa nini asifungwe kwa kushindwa kutoa fedha hizo.

Awali, Msajili Kahyoza alijitoa katika shauri hilo baada ya Shehe Mbonde kuandika barua kumtaka ajitoe kwa sababu hana imani naye. Katika barua hiyo, Shehe Mbonde ameomba msajili ajitoe kwa sababu hajaridhishwa na jinsi anavyoshughulikia shauri hilo tangu alipokee, pia kesi inavyoendelea anahisi haki aliyopewa na mahakama hiyo haitatendeka au itacheleweshwa.

Aliorodhesha baadhi ya mienendo inayomtia mashaka ikiwemo kesi hiyo kuahirishwa zaidi ya mara nane kwa sababu tofauti tofauti ikiwemo ya mawakili wa wadaiwa kutokufika mahakamani, pamoja na sababu nyingine bila kuwataka wahusika kueleza jinsi watakavyolipa fedha hizo.

Katika barua hiyo, Shehe Mbonde ameeleza kutiwa shaka na ukaribu kati ya msajili na wakili wa wadaiwa kwa kuwa amekuwa akishuhudia wakili huyo akiingia katika Ofisi ya Msajili kabla kesi haijatajwa mahakamani, jambo linalomfanya ahisi wanapanga jinsi kesi inavyokwenda.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad