Dunia imekwisha! Hiyo ndiyo
lugha nyepesi na rahisi unayoweza kuitumia kuelezea tukio hili. Januari
11, mwaka huu Tambani, Mbande wilayani Temeke jijini hapa, kijana mdogo,
Hamis Lutani Kilumbi (21) anadaiwa kumbaka mama yake mzazi, Fatuma
Mohammed Matutu (48) sambamba na kumchoma visu shingoni hali iliyomfanya
apate maumivu makali hadi kufariki dunia Januari 21, mwaka huu katika
Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Kaka wa mtuhumiwa
HII HAPA SIMULIZI YAKE
Akizungumza kwa uchungu na Amani
wakati wa mazishi ya mwanamke huyo, mtoto mkubwa wa marehemu aitwaye
Mohammed Ali, alisema kuwa siku ya tukio, mtuhumiwa ambaye ni mdogo wake
anayemfuata kuzaliwa, alifika nyumbani kwao, alipokuwa akiishi mama
yake majira ya mchana lakini hakumkuta.
“Baada ya kumkosa mama, alikuja nyumbani
kwangu maana si mbali na anapoishi mama. Lakini pia mimi, mke wangu na
mdogo wetu wa mwisho wa kike, Asma, ambaye naishi naye hatukuwepo. Kwa
hiyo, Hamis aliacha ujumbe kuwa, tukirudi tupewe taarifa yeye alifika na
mama alikuwa anatuhitaji.
Kaka wa Marehemu
UJIO WA MTUHUMIWA WATIA SHAKA
“Sasa baada ya mimi kurudi nyumbani na
kupewa taarifa hizo nilishangaa sana, kilichonishangaza si kuitwa na
mama bali ujio wa Hamis nyumbani kwangu, maana nilikuwa sijaonana naye
kwa muda usiopungua mwaka mzima kwa vile tuliwahi kutofautiana nikampiga
marufuku kuja nyumbani kwangu na yeye akaahidi akiniona popote
atanipiga na nondo,” alisema Mohammed.
…Mwili wa Marehemu ukitolewa Mochwari
Hata hivyo, Mohammed alisema baada ya
kuuliza juu ya wito wa mama yake, aliambiwa kuwa, Asma alishakwenda
nyumbani na hakuwa anawaita kama alivyosema Hamis.
Mohammed akaendelea kueleza kuwa, baada
ya maelezo hayo, aliamua kuendelea na mambo yake na alikwenda kutazama
mechi ya mpira wa miguu kati ya Simba na Yanga runingani zilizokuwa
zikicheza Zanzibar.
MLANGO WAGONGWA, WATOLEWA UJUMBE MBAYA
“Baada ya mechi nilirudi nyumbani na
kulala. Jambo ambalo sikulitegemea ni kwamba, kufika usiku wa manane,
ilikuwa yapata kama saa 8 hivi, majirani wa nyumbani kwa mama walikuja
kunigongea, wakaniambia mdogo wangu Hamis anamuua mama.
“Nilikimbia mpaka eneo la tukio.
Kiukweli nilimkuta mama akiwa na hali mbaya, alikuwa akivuja damu sana,
kitenge na kanga alizokuwa amevaa vilikuwa vimelowa damu chapachapa.”
…Mwili wa Marehemu ukitolewa Mochwari
“Niliumizwa mno na hali aliyokuwa nayo
mama. Nilimuuliza nini kilimpata na kauli yake ya mwisho alisema; ‘mdogo
wako Hamis anataka kuniua.’ Bila kupoteza muda, haraka tulimbeba mama
na kumkimbiza kwa mwenyekiti lakini hatukumkuta, tukampeleka kwa mjumbe,
akatuandikia karatasi kwa ajili ya kumkimbiza polisi.”
MAJERUHI ALALA NA MAUMIVU
Mohammed alizidi kusimulia kuwa,
kutokana na mazingira wanayoishi, haikuwa rahisi kumkimbiza muda huohuo,
wakasubiri kupambazuke kwanza na alfajiri walimpeleka kwenye Kituo cha
Polisi cha Maturubai, wakaandikiwa PF3 na kisha kumpeleka Hospitali ya
Temeke.
MADAKTARI WABAINI MAZITO
Mohammed: “Mama alifanyiwa vipimo na
madaktari walithibitisha kuwa, aliingiliwa kinyume na maumbile lakini
pia alichomwa visu shingoni. Alianza kupewa matibabu lakini hali yake
ilizidi kuwa mbaya, tukamhamishia Hospitali ya Muhimbili kwenye wodi ya
Kibasila. Bado hali ilizidi kuwa mbaya zaidi na Jumamosi ya tarehe 21,
alipoteza maisha.”
…Mwili wa Marehemu ukitolewa Mochwari
HUYU HAPA KAKA WA MAREHEMU
Naye kaka wa marehemu, Said Matutu, mkazi wa Mbagala Kokoto, Dar
alisema kuwa, amesikitishwa sana na tukio hilo lililosababisha kifo cha
dada yake na kuongeza kwamba, mtuhumiwa anatafutwa na polisi ili aweze
kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
“Kiukweli hili suala linasikitisha mno, huwezi kumfanyia mama yako
mzazi kitendo kama hicho. Huo ni unyama uliopitiliza, mtu wa namna hii
ni wa kuogopwa katika jamii,” alisema Said ambaye msiba ulifanyikia
nyumbani kwake.
…Jeneza likiandaliwa kuswaliwa.
TABIA ZA MTUHUMIWA
Hata hivyo, kaka huyo aliongeza kuwa, kabla ya tukio hilo alikuwa
akipata malalamiko kutoka kwa dada yake (marehemu) juu ya tabia za
uvutaji bangi, utovu wa nidhamu na tabia nyingine nyingi mbovu alizokuwa
nazo mtuhumiwa, lakini pia aliwahi kuambiwa kijana huyo alikuwa ni
mmoja wa vijana wahalifu maeneo ya Posta Mpya.
…Mwili ukiswaliwa
MAZISHI YAKE
Marehemu Fatuma alizikwa Jumatatu iliyopita kwenye Makaburi ya
Mbagala Mponda na ameacha familia ya watoto wanne, akiwemo mtuhumiwa.
KAMANDA WA POLISI TEMEKE
Naye Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Temeke, SSACP Gilles Muroto,
alipotafutwa na mwandishi wetu na kuulizwa kuhusu tukio hilo, alisema
taarifa hizo bado hazijamfikia lakini atafuatilia ili kujua
kilichotokea.