MKAZI wa Nsumba katika Manispaa ya Ilemela jijini Mwanza Joyce
Mathayo (33), anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa kosa la kumpiga mtoto
wake Mathayo Manisi (12) na kumuua kwa kosa la utoro shuleni.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza Ahmed Msangi akizungumza na
wandishi wa habari ofisini kwake jijini hapa jana alisema tukio hilo
lilitokea Januari 11, mwaka huu saa 4 asubuhi.
Alisema Mary alikamatwa na polisi baada ya kumpiga fimbo mtoto wake
huyo ambaye ni mwanafunzi wa darasa la tatu sehemu mbalimbali za mwili
na kumsababishia kifo, kitendo ambacho ni kosa la jinai.
Kamanda Msangi alisema siku ya tukio, mtoto huyo alimkatalia mama
yake kwenda shule na kusema hataki shule tena, ndipo mama huyo
alipopatwa na hasira na kuanza kumpiga fimbo sehemu mbalimbali za mwili
na kumsababishia kifo muda mfupi baadaye.
Alisema baada ya mtoto huyo kufa, wananchi waliamua kutoa taarifa
Kituo cha Polisi na polisi walifika mapema kwenye eneo la tukio na
kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa.
"Mtuhumiwa yupo katika mahojiano na polisi, pindi uchunguzi
utakapokamilika atafikishwa mahakamani, mwili wa marehemu umefanyiwa
uchunguzi na timu ya madaktari kutoka Hosipitali ya Rufaa ya Mkoa ya
Sekou Toure na tayari umekabidhiwa kwa ndugu wa marehemu kwa ajili ya
maziko,” alisema.
Kufuatia tukio hilo la kusikitisha, Kamanda Msangi ametoa wito kwa
wazazi kuwalea watoto wao katika maadili mema na nidhamu kwa
kuwaelimisha mambo mazuri na mabaya ili kuepusha kutoa adhabu za vipigo
kwa watoto kwa kujenga familia bora isiyo ya ukatili.