DAR ES SALAAM: INASIKITISHA
SANA! Mrembo aliyefahamika kwa jina la Queen Nazil aliyeshiriki
mashindano ya Miss Tanzania 2016 akitokea Wilaya ya Ilala jijini Dar,
hivi karibuni alikumbwa na janga kubwa baada ya kuvamiwa na watu
waliodaiwa ni vibaka kisha kumpora vitu mbalimbali kabla ya kumjeruhi
kwa mapanga, Risasi limelinyaka tukio zima.
Majeraha sehemu za kichwa cha mrembo Queen Nazil.
Rafiki wa karibu wa Queen aliyeomba jina
lake lisitajwe gazetini alisema kuwa, tukio hilo lilitokea usiku wa
wikiendi iliyopita maeneo ya Mwenge-Mpakani jijini Dar wakati mrembo
huyo akitokea kwenye mishemishe zake.
“Ilikuwa usiku wakati anatoka kwenye
mambo yake, sasa aliposhuka kwenye gari ya rafiki yake kisha ile gari
kuondoka, yeye alibaki getini akigonga ili afunguliwe lakini ghafla
ikatokea bodaboda iliyokuwa na watu wawili ambao walimpora mkoba wake.
“Sasa kwa kuwa ule mkoba ulikuwa na simu
aina ya iPhone 6, pesa shilingi laki mbili na vikorokoro vingine, Queen
alijikuta akijitetea na ndipo mmoja wa wale watu alipomkata mapanga
kichwani, akadondoka chini na kuanza kuvuja damu,” kilidai chanzo hicho.
Ikadaiwa kuwa, baada ya kujeruhiwa
walitokea wasamaria wema ambao walimchukua mwanadada huyo aliyetajwa
kuwa ni mwanafunzi wa mwaka wa tatu wa Kitivo cha Sheria, Chuo Kikuu cha
Tumaini kilichopo Mwenge jijini Dar, wakamkimbiza kwenye hospitali moja
iliyopo jijini Dar kwa ajili ya matibabu.
Risasi ndani ya Tumaini
Baada ya kuwepo kwa madai kuwa, Queen ni
mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Tumaini tawi la Dar, waandishi wetu
walifika chuoni hapo na kufanikiwa kuzungumza na Waziri wa Mawasiliano
na Habari wa serikali ya wanafunzi, Grey Paul aliyekiri kumtambua na
kwamba kweli alipatwa na balaa hilo.
“Ni kweli Queen ni mwanachuo wa hapa,
kwa mujibu wa taarifa nilizozipata alivamiwa na watu ambao wanadaiwa ni
vibaka, wakampora simu na pesa.
“Inasemekana alikuwa karibu na nyumbani
kwa dada yake aliposhushwa kwenye gari ya rafiki yake na kabla hajafika
getini alivamiwa na kuporwa vitu hivyo pamoja na kupigwa panga,” alisema
Grey.
Hata hivyo, kiongozi huyo wa wanafunzi
alisema kuwa, kwa muda huo alikuwa hajui alikokuwa akiishi Queen baada
ya kutoka kwenye hosteli za chuo hicho zilizopo Mwenge.
Risasi lilifanikiwa kupata namba ya simu
ya Queen lakini kila ilipokuwa ikipigwa ilikuwa haipatikani huku dada
mmoja aliyedai ni rafiki yake wa karibu akisema:
“Queen ni rafiki yangu mkubwa ila siwezi kuwapeleka alipo, mwenyewe hataki hili tukio likuzwe kwani litawapa presha wazazi wake.
“Ila in short (kwa kifupi) baada ya
tukio lile alipatiwa matibabu na sasa anaendelea vizuri,” alisema rafiki
huyo wa Queen aliyeomba jina lake lisiandikwe gazetini.