Ugonjwa wa homa ya ini maarufu kwa jina la hepatitis B umetajwa kuwa maambukizi yake ni makubwa na haraka zaidi ya Ukimwi.
Takwimu
za Shirika la Afya la Kimataifa (WHO) zinaonyesha kuwa kiwango cha
maambukizi ya homa ya ini B kwa Tanzania ni wastani wa watu wanane
katika kila watu 100. Maambukizi ya VVU, ni wastani wa watu watano
katika kila watu 100.
Takwimu
za wachangiaji damu katika kitengo cha uchunguzi wa magonjwa cha
Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, (MNH) kwa kipindi cha siku 14 za
Desemba 2016, zinaonyesha kuwa kati ya sampuli 480 za damu zilizopimwa,
18 zilikutwa na VVU.
Lakini,
katika sampuli 480 zilizopimwa katika kipindi hicho hicho, 56 zilikutwa
na virusi vya homa ya ini B, huku watu 20 kati yao wakiwa na ini C
(hepatitis C).
Katibu
Mkuu wa Serikali, Dk Mpoki Ulisubisya amesema Serikali imeanza
kuwatumia watafiti wake kuangalia kwa undani kasi ya maambukizi ya
ugonjwa huo.