MTOTO wa darasa la tano katika shule ya
msingi ya Engosengiu, Caren Amon (10), amejinyonga kwa kamba.
Mtoto huyo alifanya kitendo hicho kwenye
kibanda cha kufugia kuku nyumbani kwao mtaa wa Muriet kata ya Sokoni One mjini
hapa.
Caren ambaye ni mtoto wa kwanza katika
familia yao ya watoto wawili wa kike kifo chake kiliibua hisia za watu wengi
ambao walishindwa kuamini kilichotokea.
Mdogo wa marehemu, Catherine (6) aliyekuwa
akicheza na dada yake nyumbani kwao alisema wakati wanacheza, dada yake
aliokota kamba iliyoletwa na mtoto wa jirani na kumwambia mdogo wake kuwa
anataka kujinyonga.
Alisema alifanya hivyo huku mdogo wake
akijitahidi kuokoa maisha ya dada yake kwa kupanda kwenye benchi akakata kamba
na akaanguka chini na yeye kuita majirani.
Mama wa marehemu, Beatrice Mamkwe alieleza
kutoamini kilichompata mtoto wake, kwani waliagana vizuri asubuhi akienda
kazini na alishituka kupigiwa simu kuwa nyumbani kuna matatizo.
Pia aliiomba Serikali kufanya uchunguzi
wa kifo hicho ili kuondoa maswali ya sababu za mtoto huyo kujinyonga.
Baba wa marehemu, Amon Swai alisema mara
ya mwisho alizungumza na mtoto wake akimtaka asome sana kwani darasa analoingia
ni jipya na kuwa atakutana na walimu wapya na hivyo awe mtii shuleni, lakini
suala la msiba haliamini na hataki kuamini hata sasa.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Sokoni One, Petro
Mollel alisema alipokea taarifa hiyo kwa mshituko na kwamba anaiomba familia
iendelee kuvuta subira wakati uchunguzi wa chanzo cha tukio hilo kikitafutwa hasa
ikizingatiwa uamuzi huo mzito na umri wa mtoto huyo.
Majirani, Zena Ali na Mollel Joseph kwa
nyakati tofauti walisema kwa hali hiyo wazazi wanatakiwa kuwa karibu na watoto
wao kwa kuwaacha wakiwa na watu wakubwa ili kuzuia hatari zinazoweza kuepukwa.