Jinsi Mfumo wa Kieletroniki wa Malipo ya Faini za Barabarani Unavyofanya Kazi

Mfumo wa ulipaji faini za papo kwa hapo kielekitroniki unafanyakazi kama ifuatavyo:

Dereva aliyetenda kosa akikamatwa na kutakiwa kulipa faini kwa njia ya kielektroniki, askari ataingiza kwenye mashine taarifa za namba ya usajili wa gari, nambari ya leseni ya dereva, eneo kosa lilipofanyika, kosa lililofanyika na kisha askari atatoa tiketi ya kielektroniki kumpa dereva aliyetenda kosa.

Tiketi hiyo pamoja na kuwa na namba ya kumbukumbu ya malipo pia itakuwa na maelekezo kwa dereva yanayosema: Unatakiwa kulipa faini ya kosa ulilotenda kupitia mitandao ya simu ya tigo pesa, M-pesa, Airtel Money, Maxi malipo au kupitia kadi yako ya benki (ATM Card za NMB na UMOJA SWITCH).

Unatakiwa kulipa faini yako ndani ya siku saba. Baada ya siku saba utatozwa ziada ya 25%, baada ya siku kumi na nne na kuendelea utatozwa ziada ya 50% ya tozo la awali na itakuwa ikiongezeka kadiri unavyochelewa kulipa. Kwa wale watakaokamatwa wakati wa oparesheni watafikishwa mahakamani ambapo mbali na kulipa malimbikizo ya tozo watatozwa faini ya TZS 50,000/= au kifungo cha miezi miwili jela.

Ili kulipia kwa njia ya mitandao ya simu namba maalum ya Polisi (USSD Code) itakayotumika ni *152*75#. Namba hii pamoja na kutumika katika kulipia tozo pia unaweza kuangalia iwapo gari lako linadaiwa tozo la notification lililolimbikizwa.

Baada ya kutolewa tiketi hiyo dereva husika atatakiwa kulipa faini yake kwa njia hizo zilizotajwa kisha kuiwasiliha kwa askari mwenye mashine namba ya kumbukumbu ya malipo aliyoipata kupitia mtandao husika. Namba hiyo ya kumbukumbu itaingizwa kwenye mashine ya kutolea tiketi ambapo itatolewa risiti ya malipo kisha kukabidhiwa kwa dereva husika.

Ieleweke kwamba, ulipaji huu wa tozo kielektroniki hauna tofauti na ule unaotumika katika kulipia umeme wa LUKU au ada za Magari zinazotozwa kwa njia ya mtandao na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Ili kurahisisha zoezi hili la ulipaji faini kwa njia ya kielektroniki, madereva watatakiwa kutembea na leseni zao halisi za udereva vinginevyo watalazimika kupelekwa vituoni kwa ajili ya kupata taarifa zao za leseni kutoka katika computer za mfumo wa leseni za udereva jambo ambalo linaweza kuwapotezea muda.

Aidha ieleweke kwamba dereva anapoandikiwa faini ya kielekroniki akichelewa kulipa katika muda aliopewa, Jeshi la Polisi litakuwa likiendesha oparesheni mara kwa mara kwa kuyamulika magari yote yanayodaiwa faini kwa kutumia mtambo maalum wa kutambua namba za usajili wa magari yanayodaiwa (Automatic Number Plate Recognition System). Watakaokamatwa katika oparesheni hizi kwa kukwepa kulipa faini, mbali na kutakiwa kulipa faini aliyolimbikiza awali pia atafikishwa mahakamani kwa mujibu wa sharia.

ENDESHA SALAMA – OKOA MAISHA.
Imetolewa na:

MOHAMMED R.MPINGA – DCP,
KAMANDA WA POLISI,
KIKOSI CHA USALAMA BARABARANI (T)

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad