Aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila, amesema atapokelea kadi ya Chadema jimboni mwake baadaye mwezi huu.
Kafulila alitangaza kuhama NCCR-Mageuzi na kurudi Chadema kwa alichoeleza kuwa ndicho chama kilichojipambanua kuelekea safari ya mabadiliko ifikapo mwaka 2020.
Kada huyo tayari amewasilisha barua kwa Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Mosena Nyambabe kumjulisha kuwa anajivua uanachama na anarudi Chadema.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi jana, Kafulila alisema ameamua kuwa atapokelea kadi hiyo jimboni kutokana na mapenzi aliyonayo kwa wananchi wake.
"Nimepanga kuchukua kadi mwezi huu jimboni, kwa kuwa ilikuwa nichukue kadi mwanzoni lakini ilishindikana kutokana na siku kuu, hivyo siku yoyote kuanzia sasa nitachukua," alisema.
Wakati anajiuzulu NCCR-Mageuzi na kurudi Chadema, alisema hakufanya uamuzi kwa kukurupuka bali alitafakari na kushauriwa na wananchi wa jimbo lake, na kuridhika kurudi huko.
"Nilitafakari na kushauriwa sana jimboni na kuridhika kwamba Chadema ndiko sehemu inayojipambanua kwa mikakati ya kuleta mabadiliko yanayotarajiwa na Watanzania na ni vema kukusanya nguvu ya kila mwenye kiu ya mabadiliko ndani ya chama kimoja, ili kufupisha safari ya mabadiliko," alisema.
Alipoulizwa kwa nini amerudi Chadema wakati aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama hicho, Dk Wilbrod Slaa alipata kumwita sisimizi kwa alichoeleza kuwa hakuwa na imani naye, alijibu kuwa siasa ni malengo si uhusiano binafsi.
Kafulila aliongeza kuwa wanasiasa wanaunganishwa na malengo zaidi ya urafiki na kwamba malengo yake sasa ni kuendelea kupigania mabadiliko ya kimfumo yanayoenea zaidi kwenye chama hicho (Chadema) kuliko kingine.
Novemba 10, 2009 Kafulila alijivua uanachama wa Chadema na kuhamia NCCR-Mageuzi kutokana na kuondolewa kwenye nafasi ya uofisa habari wa chama hicho.
Pia akiwa NCCR-Mageuzi, alitimuliwa uanachama kwa kudaiwa kukiuka taratibu za chama hicho na tuhuma za kutaka 'kumpindua' Mwenyekiti, James Mbatia.
Hata hivyo, suala hilo lilipata suluhu baada ya Mbatia kuteuliwa na Rais mstaafu Jakaya Kikwete kuwa Mbunge. Wakiwa bungeni, Mbatia na Kafulila walikutana, kuzungumza na hatimaye kumaliza mzozo wao.