KAIMU Jaji Mkuu mpya wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma ameahidi
kuweka mkazo katika matumizi ya Tehama katika kuendesha kazi za Mahakama
kuhakikisha haki inapatikana kwa haraka.
Jaji Juma alitoa ahadi hiyo baada ya kuapishwa, tukio lililofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam jana.
Jaji Juma awali alikuwa Jaji wa Mahakama ya Rufaa Tanzania na
atashika nafasi hiyo mpaka hapo Rais Magufuli atakapofanya uteuzi wa
Jaji Mkuu.
“Katika kuwahudumia wananchi katika kutoa haki na kwa haraka
tutatumia teknolojia ya habari ili haki iweze kupatikana haraka kuliko
sasa,” alisema Jaji Juma.
Alisema alipata nafasi ya kusoma sera ya Tehama iliyotolewa Mei mwaka
jana ambayo inatoa picha ya nchi miaka 20 ijayo kuonesha nchi inatakiwa
kwenda wapi ambapo na mahakama inatakiwa kutekeleza.
“Mpango wangu ni kwamba, kesi zinasajiliwa katika mtindo huo ili
kuhakikisha haki inapatikana haraka na kwa uwazi zaidi ya ilivyo sasa,”
alisema Jaji Juma na kuwapongeza majaji wakuu waliomtangulia ambao
waliweka msingi wa mabadiliko katika mahakama ikiwa ni pamoja na kuweka
mpango mkakati unaosaidia katika utendaji kazi.
“Sheria nyingi zimebadilika, fedha nyingi zimepatikana na vilevile
mpango mkakati wa mahakama, sasa ni kuutekeleza mpango huo ….. wao
wameshamaliza kazi yao sasa ni kupunguza maneno”, alisema Jaji Juma.
Aidha alimshukuru pia Rais John Magufuli kwa kumuamini na kumteua
katika nafasi hiyo ili aweze kuwahudumia wananchi katika kutoa haki.
Rais Magufuli juzi alimteua Jaji Juma kuwa Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania
kuchukua nafasi ya Jaji Mohamed Chande Othman ambaye amestaafu.
Katika tukio hilo, Jaji Mkuu mstaafu alisema katika mambo ambayo hata
yasahau katika kazi zake ni pamoja na kubadilisha watumishi wa mahakama
kutambua kuwa ni chombo ambacho kinawajibika kwa wananchi.
“Hili ni jambo ambalo lipo na linaendelea katika kuhakikisha kwamba
mahakama ni chombo ambacho kinatoa haki na pia kwa wakati kwa Watanzania
wote,” alisema Othman na kuongeza kuwa Mahakama iko kwenye kasi ambayo
Serikali ya Awamu ya Tano inaitaka na kuwataka watendaji wanaobaki
kuongeza kasi hiyo.