Labda ulikuwa miongoni mwa watu
waliosikia taarifa ya kukamatwa kwa muuza madawa ya kulevya nchini
Mexico, JoaquÃn Guzmán Loera AKA “El Chapo Guzmán”, na ukajiuliza kuhusu
wauzaji madawa ya kulevya ambao waliwahi kutokea katika dunia hii.
Wapo wengi ambao walikuwa wauzaji wa
madawa ya kulevya, mabilionea ambao mwisho wao ulikuwa mbaya kama Pablo
Escobar. Kama ulikuwa huwajui, hii hapa chini ni orodha ya wauzaji
madawa ya kulevya hatari ambao wamewahi kuwepo katika dunia hii mpaka
sasa.
FRANK LUCAS AKA Superfly
Unapowazungumzia wauza madawa ya kulevya
ambao wamewahi kuishi katika hii dunia basi hutoweza kuliacha jina la
mshikaji huyu, Mmarekani, ‘bitozi’, bilionea ambaye utajiri wake mkubwa
ulitokana na uuzaji wa madawa ya kulevya.
Jamaa alivuma sana miaka ya mwishoni mwa
mwaka 1960 na mwanzoni mwa mwaka 1970. Jamaa alikuwa na washikaji wengi
waliokuwa wakipiga biashara hii haramu. Kila siku, alisafirisha madawa
ya kulevya kupitia kwenye majeneza ya watu aliokuwa akiwaua na washikaji
zake.
Mwaka 1975, jamaa alivamiwa nyumbani
kwake, ndani ya nyumba tu kukakutwa kiasi cha dola laki tano (zaidi ya
bilioni moja), kwa kipindi hicho, kilikuwa kiasi kikubwa sana cha fedha.
Jamaa alipokamatwa, akafungwa gerezani miaka 75 kwa kesi zaidi ya 100
za madawa ya kulevya.
CHRISTOPHER COKE AKA: “Dudus”
Jamaa alikuwa mpiga dili mkubwa tu
kwenye biashara ya madawa ya kulevya. Alikuwa Mjamaika, mwenye sura ya
kipole, kusaidia watu ambapo baada ya kugundulika kwamba anafanya
biashara hiyo, hakutaka hata kutafutwa, mwenyewe akajipeleka polisi
mwaka 2010.
Mshikaji aliingiza kiasi kikubwa cha
fedha, mpaka kukamatwa kwake alikuwa ameingiza kiasi cha dola bilioni 30
(zaidi ya trilioni 60) ambapo kwa sasa tungesema kwamba yeye ni tajiri
wa 18 duniani.
Japokuwa alikuwa na ubaya wake wa
kufanya biashara hiyo haramu lakini mshikaji alikuwa mtu wa watu.
Alikuwa akijenga hospitali, kufanya biashara nyingine na kuwaajiri watu
wengi, aliwasaidia masikini na kuwafurahisha kwa kuyaboresha mazingira
yao japokuwa upande wa nyuma, aliteketeza vijana kwa kuwauzia biashara
hiyo.
GRISELDA BLANCO AKA: “The Cocaine Godmother”
Unaweza kumchukulia poa tu kwa sababu ni
mwanamke lakini ni lazima ujue kwamba kwa watu waliokuwa wakifanya
biashara ya kulevya kwa kiasi kikubwa huwezi kumuacha huyu mwanamke.
Alikuwa mtu wa dili, mbali na uuzaji wa
madawa hayo, pia alikuwa muuaji mzuri tu ambaye kwa kipindi chote cha
kufanya biashara yake, aliwaua watu 200 kwa risasi, tena kwa mkono wake
mwenyewe.
Baada ya kufanya biashara hiyo kwa miaka
kadhaa, akakamatwa na kufungwa miaka 20 gerezani, ila cha kushangaza
sasa, akiwa hukohuko nyuma ya nondo, michongo yake ya biashara ilikuwa
ikisonga kama kawa.
Mwaka 2004 akatolewa gerezani lakini
ilipofika mwaka 2012, akauawa kwa kupigwa risasi na mshikaji aliyekuwa
akiendesha pikipiki. Huo ukawa mwisho wake, akazikwa ingawa bado
anajulikana kama mfanyabiashara mkubwa wa biashara hiyo haramu.
Rick Ross AKA: “Freeway”
Siyo huyu unayemjua wewe! Siyo yule
jamaa mwenye mwili mkubwa, mwanamuziki wa Kimarekani, achana na huyo,
mshikaji mwenyewe alilichukua jina la Rick Ross kutoka kwa huyu jamaa.
Mwili mdogo, mtanashati, alipenda
kutabasamu lakini nyuma ya tabasamu lake, jamaa alikuwa ‘mbaya’ kwenye
biashara ya madawa ya kulevya.
Jamaa alianza kufanya biashara hiyo
miaka ya 1980. Alianza kama ‘punda’ yaani mbebaji lakini baadaye
akajizatiti na kuwa na biashara yake mwenyewe. Jamaa alikuwa akiuza
mzigo wa dola milioni 3 (zaidi ya bilioni 6) kila siku iendayo kwa
Mungu. Mshikaji alikuwa akiuza kilo 400 kila wiki.
Arturo Beltrán Leyva AKA: “Boss of Bosses”
Kama washikaji wa hapo juu, hata huyu
mwana alikuwa nuksi kwenye uuzaji wa madawa ya kulevya. Mshikaji alikuwa
na kundi lake liitwalo Beltran Leyva Cartel, kundi lililosumbua sana
nchini Mexico.
Kulikuwa na kesi nyingi dhidi ya kundi
hilo, watu walikuwa wakiuawa, wanawake walibakwa, walisafirisha sana
silaha kwenda sehemu mbalimbali, wengine waliteswa na kutekwa. Kwa
kifupi, kundi hili lilikuwa hatari zaidi kuliko makundi mengine
yaliyowahi kutokea huko.
Jamaa aliuawa na wanajeshi wa majini mwaka 2009 katika majibizano ya kurushiana risasi na wanajeshi hao.
Felix Mitchell AKA: “The Cat”
Jamaa alikuwa si kitoto, huyu ni
miongoni mwa wauza madawa ya kulevya wakubwa waliowahi kutokea duniani.
Alikuwa na kundi lake liitwalo 69 Mob. Jamaa alikuwa akipiga dili za
chinichini, ilikuwa vigumu kukamatwa kwani alikuwa mjanja kupindukia.
Alipokamatwa, alifungwa jela miaka mingi
tu ila wakati akiwa ametumikia kifungo kwa miaka miwili, kuna jamaa
hukohuko jela akamuua kwa kumchoma kisu, hiyo ilikuwa mwaka 1986 na
mazishi yake yalihudhuriwa na watu wengi, sawa na mazishi ya aliyekuwa
mwanaharakati, Martin Luther King Jr.
Amado Carrillo Fuentes AKA: “Lord of the Skies”
Alikuwa Mmexico aliyekuwa akifanya
biashara ya madawa ya kulevya kwa kiasi kikubwa. Hakuwa mkuu wa kitengo,
aliajiriwa na bosi wake aliyeitwa Rafael Aguilar Guajardo ila akaamua
kumuua na kushikilia yeye hicho kitengo.
Ndiye muuzaji pekee wa madawa ya kulevya aliyekuwa akiingiza kiasi kikubwa nchini Marekani kuliko mtu yeyote.
Alikuwa bilionea, mwenye kupenda watu na
kusaidia masikini. Hakuwa na utani katika biashara hiyo, aliua wote
aliohisi kwamba walikuwa watu wabaya katika biashara yake.
Alitumia ndege zake kusafirisha madawa
ya kulevya kwenda nchini Marekani mara nne kwa siku. Kumkamata haikuwa
kazi nyepesi kwa sababu alikuwa akibadilisha sura yake kwa kuvaa sura ya
bandia.
Mwaka 1997 alipokuwa akifanyiwa upasuaji
wa kuwekewa sura ya bandia katika Hospitali ya Santa Monica nchini
Mexico, dawa zilizidi hivyo kufariki dunia na baada ya siku mbili, wale
madaktari waliofanya upasuaji huo wa kumuwekea sura ya bandia wakakutwa
wameuawa kinyama na miili yao kutupwa.
Pablo Escobar AKA: “The World’s Greatest Outlaw”
Huyu jamaa alikuwa kiboko, ni Mcolombia
aliyekuwa akiuza madawa ya kulevya kwa kiasi kikubwa. Alikuwa katili,
kuua watu waliokuwa kinyume naye ilikuwa ishu ndogo sana kwake.
Hakutaka mchezo, hakuwahi kuweka fedha
benki, alikuwa akizihifadhi ndani na wakati mwingine zilikuwa zikiliwa
na panya. Kuna kipindi mtoto wake alikuwa akiumwa, alizitumia dola za
Kimarekani kumuwashia moto, eti kupoza baridi lililokuwa likimpiga,
kitu kilichowakasirisha sana Wamarekani, waliona wamedharauliwa sana
mpaka noti yao kuchomwa moto.
Alikuwa na utajiri mkubwa na mwaka 1989
alitangazwa kama tajiri wa saba duniani akiwa na utajiri wa dola bilioni
25 (zaidi ya shilingi trilioni 50). Jamaa alikuwa akimiliki 4/5 ya soko
kubwa la madawa ya kulevya duniani.
Jamaa alikuwa akisafirisha tani 15 za
madawa ya kulevya kila siku barani America. Jamaa aliua majaji 30
waliokuwa wakisimamia kesi zake na polisi 400 ambao walionekana
kimbelembele kumfuatilia kwenye mishe zake na pia aliilipua ndege aina
ya Avianca Flight 203 ambayo ilikuwa ikimbeba waziri mkuu wa kipindi
hicho nchini Colombia.
Kwa kifupi, jamaa alikuwa na pesa ndefu
kiasi cha kuiambia serikali yake kwamba imuache afanye mishe zake kwani
angelipia deni la dola bilioni 20 (zaidi trilioni 40) lililokuwa
ikidaiwa, ila serikali ikakaata na kumuua.
JoaquÃn Guzmán Loera AKA “El Chapo Guzmán”
Hapa ndipo kwenye kazi sasa. Huyu
anaonekana kama mwamba wa biashara hii ya madawa ya kulevya. Ni Mmexico
mwenye mkwanja mrefu ambapo amekuwa akiupata kupitia biashara yake
haramu.
Alikuwa mtu anayetafutwa kwa nguvu zote
kabla ya kukamatwa. Aliwekeza nguvu kubwa katika biashara hii,
Wamarekani na Wamexico walimtafuta lakini hawakumpata.
Wakati wakiwa na uchungu naye,
wakafanikiwa kumpata na hivyo kufungwa nchini Mexico. Kutokana na fedha
alizokuwa nazo, inasemekana kwamba aliwahonga askari magereza na
kutoroka kwa kupitia katika bomba la choo, unaamini hilo?
Wamarekani walikasirika sana, wakaahidi
kumtafuta, kweli wakaingia mzigoni. Hawakuchukua muda sana, wakamnasa na
hivyo kuiambia Serikali ya Mexico kwamba watamfunga wao wenyewe ili
wamuonyeshee kwamba wao si watu wa mchezo, kweli wakamfunga na mpaka leo
hii yupo gerezani akiendelea kutumikia kifungo chake ambacho
hakikuwekwa wazi ni cha muda gani.