Kesi ya uchochezi inayomkabili Mbunge wa Singida Mashariki
(Chadema), Tundu Lissu, leo imeshindwa kusikilizwa kwa mara nyingine
kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi, Kisutu na kupigwa kalenda hadi Februari
14, 2017.
Akisoma maelezo ya kesi hiyo, mbele ya Hakimu Mkazi, Godfrey
Mwambapa, mwendesha mashtaka wa serikali aliiambia mahakama kwamba
shahidi wa jamhuri aliyepaswa kuwasilisha ushahidi wake leo dhidi ya
mbunge huyo ambaye pia ni mwanasheria mkuu wa Chadema, amepata dharura
ya kikazi.
Baada ya kuridhishwa na maelezo hayo, hakimu Mwambapa aliiahirisha kesi hiyo ambayo inatarajiwa kusikilizwa tena, Februari 14.
Lissu anakabiliwa na mashtaka ya kudaiwa kutoa maneno ya uchochezi
dhidi ya mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Pombe
Magufuli, Juni 28, 2016.
Wakati huohuo, kesi nyingine inayomkabili Lissu, wahariri wa Gazeti
la Mawio, Simon Mkina na Jabir Idrisa na mchapishaji wa gazeti hilo,
Ismail Mahbood ambayo leo ilifikishwa mahakamani kwa ajili ya
usikilizwaji wa awali, imeahirishwa hadi kesho, Januari 19, 2017.
Kwa mujibu wa wakili wa serikali, Patrick Mwita mbele ya Hakimu Mkazi
Mkuu,Thomas Simba, aliomba kesi hiyo isikilizwe siku nyingine kutokana
na kutokamilika kwa maelezo ya awali ya kesi hiyo.