Waziri Mkuu Kassim
Majaliwa amesema Serikali imeruhusu tani milioni 1.5 za chakula
zilizokuwa zimehifadhiwa zianze kuuzwa ili kukabiliana na kupanda kwa
bei za vyakula.
Pia,
Majaliwa amesema kupanda kwa bei ya vyakula nchini kulichangiwa na
ukosefu uliojitokeza nchi jirani, lakini akawataka wananchi wasiwe na
hofu kwani chakula kipo cha kutosha.
Kauli
ya Waziri Mkuu imekuja wakati mjadala wa upungufu wa chakula nchini
ukizidi kupamba moto na kusababisha baadhi ya wadau kudai kuwa, Serikali
inachelea kutangaza kuwa kuna njaa nchini.
Tayari,
Rais John Magufuli ameshaeleza kuwa hakuna baa la njaa na kama
litatokea, yeye ndiye pekee mwenye mamlaka ya kutangaza na kufafanua
kuwa tatizo hilo linakuzwa na wafanyabiashara wachache na wanasiasa
wanaotaka kujinufaisha na hali hiyo.
Jana,
Majaliwa aliyezungumza na waandishi wa habari baada ya kuwasili mjini
hapa na ndege ya kwanza ya Bombadier kufanya safari za kibiashara kati
ya Dar es Salaam na Dodoma, alisema hali ya upatikanaji chakula nchini
ni tofauti na inavyoelezwa na baadhi ya vyombo vya habari.