Kudadeki..Kumbe Daraja la Kigamboni Linaingiza Pesa Ndefu Kiasi Hiki..!!?


SHIRIKA la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) limekusanya Sh. bilioni sita za tozo ya kivuko kwa miezi nane, katika daraja la Mwalimu Nyerere, Kigamboni, jijini Dar es Salaam.

Makusanyo hayo, imeelezwa, ni kuanzia katikati ya Mei, mwaka jana hadi mwezi huu na ni juu ya lengo kwa asilimia 20.

NSSF inakuwa taasisi ya pili ndani ya wiki moja kutangaza mapato ya mradi, baada ya Mabasi Yaendayo Haraka jijini Dar es Salaam (Dart) kufanya hivyo Alhamisi.

Akizungumza na Nipashe jana juu ya maendeleo ya mradi wa daraja hilo, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Profesa Godius Kahyarara alisema limeingiza jumla ya Sh. bilioni sita.

Aidha, Prof. Kahyarara alisema gharama za uendeshaji wa daraja hilo katika kipindi hicho ni jumla ya Sh. milioni 800 tu.
Prof. Kahyarara alisema NSSF imemudu kuvuka lengo kwa wastani wa asilimia 20 kutokana na kutumia waajiriwa wake badala ya wakala.

Alisema awali makaridio yalikuwa ni kukusanya Sh. bilioni tano katika kipindi hicho.

“Sera yetu ni kwamba hizi fedha hatuzitumii," alisema Prof. Kahyarara."

"Tunaziwekeza moja kwa moja BoT (Benki Kuu) katika mnada wa dhamana za serikali (treasury bonds) ambayo ni ya asilimia 13.5 ambayo ikiiva miaka 15 ijayo ni Sh. bilioni 18."

Alisema kwa uwekezaji huo, NSSF itarudisha fedha zilizojenga daraja na faida ya kutosha.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, kwa utaratibu wa BoT kila baada ya miezi sita wanaweza kuvuna faida ambayo watawekeza kwenye miradi mingine ya maendeleo.

“Utaratibu huu tumeona unalifanya Shirika kuwa na uhakika, kwamba likihitaji fedha ya haraka wanaweza kuzitumia na taarifa zitaonyesha fedha za daraja zilishapatikana. Ni ubunifu tulioanzisha kwa kuwa tuliona ukiweka sekta binafsi huwezi kupata faida hiyo,” alifafanua.

Aidha, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF alisema iwapo kazi ya kukusanya fedha hizo ingepewa kampuni binafsi wangepata hasara ya Sh. milioni 300.

Prof. Kahyarara alibainisha kuwa NSSF ilitaka tangu siku ya kwanza ya kutumika kwa daraja hilo faida ianze kukusanywa jambo ambalo limefanikiwa kwa kiasi kikubwa.

"Tuna uwezo mkubwa wa kukusanya fedha, tuna madirisha ya kutosha na watu wenye utaalamu kama walioko mabenki. Itakuwa ni kituko kumuita mtu kutukusanyia fedha, hivyo hatuna mpango wa kutumia kampuni binafsi," alisema Prof. Kahyarara.

"Kwa kutumia wafanyakazi wetu wenyewe tuna uhakika mkubwa wa kukusanya zinazoingia na kurudisha fedha zetu kwa wakati.”
Prof. Kahyarara alisema kazi ya NSSF ni kuandikisha wanachama, kukusanya fedha za wanachama, kulipa mafao na kuwekeza ili fedha ziwe na thamani zisikae bila kuwa na thamani.

Ujenzi wa daraja hilo, ambao uligharimu dola za Kimarekani milioni 128, ulianza mwaka 2012 na kufanywa na kampuni ya China Railway 15 Group ikishirikiana na kampuni ya China Bridge Engineering Group.

Daraja hilo lililozinduliwa Aprili 19, mwaka jana, na Rais John Magufuli, lina urefu wa mita 680 na jumla ya barabara sita.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad