WAZIRI Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba,
amesema zipo kila dalili ya nchi kukumbwa na upungufu wa chakula, hivyo wanasiasa
bila kujali itikadi zao, wanapaswa kuungana kubuni mikakati na hatua za
kuchukua kudhibiti hali hiyo.
Akizungumza na gazeti hili jana, Mwenyekiti
huyo wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba alisema si sahihi kuendelea
kubishana kuwa nchi ina njaa au haina, wakati dalili zinaonesha uwezekano wa
kukumbwa na upungufu wa chakula.
“Watanzania tuwe pamoja kulikabili hili
kama tulivyokuwa tukifanya huko nyuma. Hili ni suala la kitaifa, ni lazima
tuungane kujua wakati huu tunafanya nini na hali ikiharibika tufanye nini,
tusilifanye suala hili kuwa la kisiasa,” alionya Jaji Warioba.
Alisema nchi kukumbwa na upungufu wa
chakula ni jambo la kawaida na si jipya, kwa vile limekuwa likitokea miaka ya
nyuma kutokana na sababu mbalimbali, ikiwamo mvua kutonyesha kwa wakati.
Huku akieleza jinsi Rais wa Awamu ya Kwanza,
Julius Nyerere alivyokuwa akihimiza wananchi kulima na kuhifadhi chakula
ikitokea nchi inakumbwa na upungufu wa chakula, alitaja mambo manne yanayopaswa
kufanyika ili kukabiliana na kadhia hiyo.
Sakata la nchi kukumbwa na njaa
liliibuka katika maeneo mbalimbali huku vyombo vya habari vikiripoti taarifa za
wananchi kushindia maembe na mifugo kufa, kutokana na ukame.
Wanasiasa na wasomi walizungumzia jambo
hilo na kuitaka Serikali kuchukua hatua za haraka huku viongozi wa dini
wakienda mbali zaidi na kuwataka waumini wao wafanye hija, mfungo, mikesha na
maombi ili kunusuru hali hiyo.
Jumatatu wiki hii, Waziri Mkuu Kassim
Majaliwa alisema Serikali itagawa tani milioni 1.5 za chakula zilizobaki msimu
uliopita katika maeneo yenye uhitaji mkubwa ili kupunguza kasi ya ongezeko la
bei za vyakula nchini, lakini akakana taarifa kuwa nchi ina njaa.
Wakati Majaliwa akitoa ufafanuzi huo,
Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk Charles Tizeba, alisema Serikali kupitia
Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), katika mwaka wa fedha wa 2016/17
imepanga kununua tani 100,000 za chakula, na hadi Januari 8, wakala huyo
alikuwa amenunua tani 62,087 za mahindi.
Lakini jana, Jaji Warioba alisema licha
ya nchi kujitosheleza kwa chakula kuna baadhi ya maeneo yana upungufu unaosababisha
utegemezi wa chakula kutoka sehemu zingine za nchi.
“Ndiyo maana tumekuwa na mikoa ambayo
inasikifika kwa uzalishaji chakula. Lakini mwaka huu kwa dalili hizi na mambo yanayoambatana
na mabadiliko ya tabianchi, inaonekana kutakuwa na upungufu wa chakula kwa
sehemu kubwa,” alisema.
Aliongeza, “hii inatokana na mvua
kutonyesha kama inavyotarajiwa. Hili si jambo jipya limewahi kutokea miaka ya
nyuma.”
Alisema kwa kuwa kuna dalili za upungufu
wa chakula ni lazima kujiandaa kukabiliana na hali hiyo, ikiwamo kuhadharisha
wananchi.
“Pia lazima kusaidia wananchi kutumia
njia zitakazowawezesha kupata mazao. Hilo linapaswa kufanywa na Serikali na
watu wa kada mbalimbali. Hapa wananchi wanaweza kupewa elimu au mbegu
zinazostahimili ukame,” alisema.
Alisema, “bado tuna muda maana kuna
sehemu ambazo zinapata mvua za vuli. Licha ya mvua kutonyesha kama
ilivyozoeleka, wananchi washauriwe kuzitumia vizuri, ni wajibu wa Serikali kusaidia
wananchi hata kama wanahitaji mbegu.”
Kwa mujibu wa Jaji Warioba, nchi
inapokumbwa na upungufu wa chakula, wananchi pia wanapaswa ama kulima au
kuhifadhi chakula na si kusubiri Serikali ishughulikie suala hilo.
“Nakumbuka mwaka fulani nchi ilikumbwa
na upungufu wa chakula, Serikali iliwataka wananchi walime. Nakumbuka Nyerere aliwaeleza
wananchi walime, la sivyo tutakufa na watu walilima kila mahali,” alisema na
kuongeza:
“Wenye uwezo wanunue chakula na
kukitunza. Haifai tuanze kulumbana, maana mwisho wa siku Serikali itajitahidi
kuziba pengo la upungufu kama upo,” alisema.
Aliongeza kuwa viongozi bila kujali
vyama, jambo la kwanza wanalopaswa kufanya ni kuhimiza wananchi watumie mvua
zinazonyesha sasa kupanda mazao, pili, kutathmini hali ilivyo na kama itatokea
waamue watafanya nini.
Alisema si sahihi kuendelea kubishana
kuwa nchi ina njaa au haina njaa, wakati dalili zinaonesha uwezekano wa
kukumbwa na upungufu wa chakula.
“Watanzania tuwe pamoja kulikabili hili,
kama tulivyokuwa tukifanya huko nyuma. Hili ni suala la kitaifa hivyo ni lazima
tuungane,” alisema.