Mkuu wa kamati ya bajeti katika bunge la Kuwait, Adnan Abdulsamad ametahadhrisha kuwa hivi sasa kuna walimu wanne tu nchini humo wanaofundisha somo la Fizikia na kusisitiza kuwa idadi hiyo haikubaliki kwa namna yoyote.
Waziri wa Elimu ya Juu wa Kuwait Muhammad Al-Faris naye pia ameashiria uhaba mkubwa wa walimu ilionao nchi hiyo katika masomo muhimu kama Fizikia na Hesabati na kupendekeza kuwa ili kukabiliana na tatizo hilo serikali iwaajiri Wakuwaiti wasio na vitambulisho vya uraia wanaojulikana kama 'Bedoons'; kwa kuzingatia kuwa wengi miongoni mwao wanafaulu kwa kiwango cha juu lakini kutokana na utambulisho wao, vyuo vikuu vya nchi hiyo haviko tayari kuwapatia fursa za kuendelea na masomo ya juu.
Akizungumzia suala hilo, Abdulsamad amesema ni heri kuwapa mafunzo na kuwatumia Bedoons kuliko kuajiri walimu kutoka nje ya nchi kwa ajili ya kutatua tatizo la uhaba wa walimu.
Nchini Kuwait kuna idadi ya Waarabu zaidi ya laki mbili waishio majangwani wanaojulikana kama Bedoons. Serikali ya Kuwait inawachukulia waarabu hao kuwa ni watu wasio na utambulisho na haiko tayari kuwapatia uraia wa nchi hiyo…/