Katika hali isiyokuwa ya kawaida na kushangaza, wananchi wa Kijiji cha Rokili, Halimashauri ya Wilaya ya Siha mkoani hapa, wapo kwenye mshangao kufuatia tukio la Kennedy Josia Nkini (18), kukumbwa na ugonjwa wa ajabu uliomsababisha kuwa mfupi ghafla.
Akizungumza na Gazeti la Amani juzi, mama mzazi wa mtoto huyo, Mary ambaye pia ni mgonjwa, alisema mwanaye alizaliwa mwaka 1999 akiwa mzima wa afya ambapo aliendelea kukua vizuri hadi alipofikisha umri wa miaka 11 (2006), kipindi hicho akiwa mrefu tu, akaanza darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Rokili iliyopo Siha.
Mama huyo alisema familia ni ya watu warefu sana hivyo mwanaye akiwa na miaka 10 tu tayari alikuwa mrefu, sasa katika hali ya kushtua, siku moja mwanaye aliporudi shule alianza kunyonyoka nywele kichwani na kuwashwa na kila alipojikuna nywele zilitoka. “Nilimuuliza labda ameiba maparachichi ya watu shambani akakataa, akasema hali hiyo ilimtokea ghafla.
Ndipo nilipompeleka Hospitali ya KCMC Moshi ambako alilazwa kwa ajili ya uchunguzi. “Siku iliyofuata asubuhi, niliitwa chumba cha daktari na kuulizwa mtoto wangu alikula chakula gani? Nikawaambia sikumpa chochote, wakanipeleka kumshuhudia.
“Nilipigwa butwaa baada ya kumuona mwanangu. Hakuwa tena yule niliyeingia naye usiku wa jana yake, alikuwa mfupi kupita kiasi. Nilishangaa sana. Nikaangua kilio nikiwauliza madaktari kulikoni mwanangu amekuwa vile?
Na wao hawakujua kilichotokea,” alisema mama huyo. Mama huyo alisema, mtoto wake aliendelea kulazwa KCMC miezi nane akimuuguza ambapo tayari ngozi yake ilikuwa imebadilika na kuwa na magamba kama ya mnyama, miguu ikizidi kuwa midogo kama ya mtoto na kukosa nguvu ya kutembea.
Alisema madaktari walijitahidi kumsaidia mtoto huyo lakini ikashindikana, hatimaye walimruhusu kuondoka naye kwa ajili ya kwenda kujaribu dawa za miti shamba ambazo pia hazikumsaidia.
Mama alisema, licha ya Kennedy kuwa hivyo, waliona aendelee na shule lakini na yeye mtoto licha ya maumivu makali, alipenda kusoma hivyo waliongea na walimu wa shule na kumruhusu kuendelea kusoma licha ya kwamba kulikuwa na hali ya kutengwa na baadhi ya wanafunzi wenzake ambao walikuwa wakimuogopa.
“Baba yake anaitwa Josia Zefania Nkini ana miaka 59, alipata kazi ya ziada ya kumbeba mgongoni kumpeleka shuleni umbali wa kama kilomita tatu na alitakiwa kumpeleka asubuhi na jioni kumfuata hadi alipomaliza darasa la saba mwaka jana na kufanikiwa kufaulu.
Hapa anatakiwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka huu.” Kijana huyo amefaulu kutoka Shule ya Msingi Rokili ambayo ipo mlimani lakini sekondari aliyopangiwa kwenda ni ya Suumu, pia ipo Halmashauri ya Siha na ipo mlimani juu kabisa ambapo kwa hali aliyonayo itakuwa ndoto kufika huko.
Kilio cha majirani, familia ya kijana mwenyewe ni kwa Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Said Mecky Sadick wamsaidie kumtafutia shule itakayoendana na hali yake.
Amani lilifanikiwa kuongea na kijana Kennedy ambaye licha ya hali yake lakini yeye anaona kawaida na anajichukulia kama binadamu wengine na ni mcha Mungu kwani hata Amani mara baada ya kufika nyumbani kwao, kabla ya mazungumzo alianza kumpa Mungu utukufu kwa kusali ndipo maongezi yaliendelea.
Alisema: “Kaka mimi nimeshakubaliana na hii hali ya ulemavu ingawa bado nina tumaini siku moja Mungu anaweza kuniokoa na nikarejea kama zamani pamoja na urefu wangu, lakini kinachonipa mawazo muda mwingi ni kuhusu kusoma.
Napenda sana kusoma ndiyo maana hata darasani nimekuwa mtu wa kumi na kufanikiwa kufaulu.”
“Naiomba serikali kupitia kwa waziri wa elimu inisaidie kunipatia shule ya walemavu, lakini nguo sina, baiskeli yangu imeisha, matairi yalishapasuka mwaka wa tatu sasa na mama yangu anaumwa mwaka wa pili huu,” alimaliza kusema.