Magari yenye taa za mwanga mkali yapigwa marufuku

POLISI Kikosi cha Usalama Barabarani kimesema kitaanza kukamata magari yote ambayo yamewekwa taa zenye mwanga mkali (spotlights) kwa kuwa uwekaji wa taa hizo, ni kinyume na sheria ya usalama barabarani.

Uwekaji wa taa hizo zenye mwanga mkali, umezuka kwa kasi katika maeneo mbalimbali nchini, jambo ambalo limetajwa linaweza kusababisha ajali kwa dereva atakayemulikwa na taa hizo.

Kauli hiyo imetolewa na Kamanda wa Kikosi hicho, Naibu Kamisha Mohammed Mpinga wakati akizungumza na gazeti hili ofisi kwake jijini Dar es Salaam, ambapo alisema ukamataji wa magari hayo utaanza rasmi wiki ijayo.

Mpinga alisema wameshatoa maelekezo kwa askari wa usalama barabarani, kuhakikisha wanakamata magari, pikipiki na malori makubwa ambayo yamewekwa taa hizo.

“Ziko taa za aina fulani zinazowekwa kwenye magari na hata ukitembea usiku utaona mwingine ameweka taa moja mwingine anaweka nyingi sana, kiasi ambacho zimeleta matatizo kwa madereva wengine,” alisema Kamanda Mpinga.

Aidha, alisema kwenye barabara kuu kuna mtindo wa madereva wa magari makubwa, kuweka taa kubwa ambazo zinawekwa juu na kumulika mwanga mkali, kiasi ambacho dereva anayemulikwa anapata upofu wa muda na kushindwa kudhibiti chombo chake.

Kamanda Mpinga alisema kuwa walishatoa muda wa kutosha kwa wamiliki wote wa magari, walioweka taa hizo kuziondoa, hivyo kwa sasa wataanza kuwachukulia hatua wote ambao watakuwa hawajaziondoa.

Alifafanua kuwa uwekaji wa taa hizo ni kinyume cha Sheria ya Usalama Barabarani Kifungu cha 39 Sura ya 168, ambacho kinaeleza matumizi ya taa. Mpinga pia alisema magari yatakayokamatwa ni yale ambayo yameongezewa taa hizo.

Alisema magari ambayo yametoka kiwandani yakiwa na taa hizo, hayatahusika.

“Hapa nazungumzia taa za kuongeza. Lakini pia kuna magari kwa ajili ya uwindaji huwa yanawekwa taa, lakini wanachotakiwa kufanya waweke kava, wakati wote ziwe na kava,” alisema.

Alisema wamiliki wa magari hayo ya kuwindia, wanatakiwa kuondoa kava hizo wanapokuwa porini tu na kuongeza kuwa mtindo wa wamiliki wa magari makubwa kuweka taa nyuma ya magari ambayo inamulika, matokeo yake mtu anayemfuata anafikiri gari anakuja kumbe inakwenda mbele.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad