Maiti ya mtoto Haruna Kyando (9) ambayo ilikutwa nyumbani muda mfupi baada ya wananchi kutoka makaburini kumzika, imezikwa kwenye makaburi ya Isanga chini ya ulinzi wa askari wa Jeshi la Polisi nchini, huku waombolezaji wakiaga mwili huo kwa kufunuliwa jeneza eneo la kichwani makaburini hapo.
Aidha, Mchungaji wa Kanisa la Bonde la Baraka, ameingizwa lawamani kwa kupotosha umma.Haruna aliyekuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa kifafa tangu udogo wake, alikutwa na wazazi wake Jailo Kyando (36) ambaye ni muosha magari na mkewe, Anna Elieza (32) akiwa amefia usingizini Jumatatu wiki hii nyumbani kwao Mtaa wa Igoma A, Kata ya Isanga jijini Mbeya.
Kilichowapa taharuki wakazi wengi jijini hapa ni baada ya ndugu, jamaa na marafiki wa familia ya Haruna walipotoka makaburini siku hiyo walikokwenda kuzika, waliporejea nyumbani waliukuta mwili wa mtoto huyo ukiwa umelazwa kwenye godoro, pale pale ulipowekwa wakati walipokuwa wakiuandaa kuuweka kwenye jeneza.
Jeneza baada ya kufukuliwa kutoka kaburini.
Hatua hiyo ilizua taharuki kubwa kiasi cha wananchi kutaka kufahamu
ni kitu gani kilichozikwa ndani ya jeneza na ndipo Jeshi la Polisi
lilipoingilia kati, kuzuia kufukuliwa kwa kaburi husika.Hatua hiyo ilisababisha vurugu na hatimaye saa tatu za usiku siku hiyo hiyo ya maziko ya awali, Polisi wakalazimika kutumia mabomu ya machozi, kutawanya watu waliofurika katika makaburi ya Isanga wakishinikiza kaburi lifukuliwe.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Igoma pamoja na Baba wa Marehemu wakifunua jeneza kuhakikisha kama kulikuwa na mwili wa marehemu.
Shughuli hiyo iliyodumu kwa muda wa nusu saa kama ilivyokuwa siku ya kwanza, ilihudhuriwa na mamia ya wakazi jijini hapa waliotaka kujua nini kilichozikwa ilhali mwili ukiwa umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya kwa wakati huo.
Jeneza lililofukuliwa likiwa halina kitu ndani yake.
Nusu saa baadaye jeneza la mtoto huyo lilitolewa nje ya kaburi na
ndipo Mwenyekiti wa Mtaa wa Igoma A, Fredy Mwaiswelo alipofunua jeneza
na kukuta ndani kukiwa tupu, hali iliyoashiria mwili wa marehemu
haukuwekwa ndani ya jeneza wakati wanakwenda kuzika.
Kutokana na hali hiyo, Polisi kwa
kushirikiana na baadhi ya vijana, walibeba jeneza hilo na kuelekea nalo
katika Kituo cha Polisi kwa ajili ya uchunguzi zaidi kabla ya
kuwakabidhi tena wanandugu mwili ili kuendelea na taratibu za maziko kwa
mara nyingine.
Baada ya ndugu kukabidhiwa mwili,
jeshi hilo pia lilisimamia maziko yaliyofanyika upya saa 10 jioni katika
kaburi lile lile la awali, lakini tofauti na awali, kabla ya kuzika
ulifanyika utaratibu wa ndugu, jamaa na marafiki waliohudhuria, kuuaga
mwili wa marehemu uliokuwa ndani ya jeneza lililofunuliwa upande wa
kichwani.
Kutokana na mkanganyiko uliojitokeza,
baadhi ya ndugu na majirani wa Mtaa wa Igoma, walisema tukio hilo
linaweza kuwa na sura mbili kwa maana ya hujuma iliyofanywa kwa
makusudi, ikilenga maslahi binafsi ya mtu inayohusishwa na imani za
kishirikina au bahati mbaya ya kuusahau mwili wa marehemu.
Walisema inaweza kuwa hujuma kutokana
na kawaida ya misiba kabla ya maziko, lazima ndugu watoe heshima za
mwisho kwa marehemu, lakini kwa msiba huu haikufanyika pamoja na baadhi
ya ndugu kutohudhuria mazishi.
Akizungumza nyumbani kwake jana
pamoja na kukanusha tuhuma za kuhusisha tukio hilo na imani za
kishirikina, baba wa marehemu alisema mkanganyiko uliojitokeza wakati
taratibu za kuuandaa mwili zikifanyika pamoja na uzushi uliofanywa na
mchungaji, ambaye alisema hamjui kwa jina, ndiyo vilivyokuza jambo hilo.
Alisema kama ilivyo kawaida baada ya
majirani kupata taarifa za msiba wakiwa nyumbani hapo, walichanga fedha
na kutuma watu kwenda kununua jeneza.
“Wananchi walichanga hela wakanunua
jeneza likaletwa nyumbani. Waliobeba jeneza walilisukumiza tu kwenye
chumba wakatoka, sisi tukaendelea na taratibu nyingine za mazishi.
Baadaye akaja mwenyekiti akasema toeni mwili wa marehemu nje, wakatoa
meza nje wakatuma vijana waende kuchukua mwili wa marehemu ndani.
Waliopeleka jeneza ndani na waliokwenda kulichukua ni watu wengine.
Jeneza likawekwa juu ya meza tukaendelea na mahubiri,” alisema Kyando.
Alisema baadaye walikwenda kuzika na
baada ya kuzika walirudi nyumbani kisha wakala chakula na kunawa maji,
kama ilivyo desturi ya misiba mingi mkoani hapa.
“Tumenawa maji tukakaa. Baada ya
kukaa kuna mgeni akaingia katika chumba tunacholala ambapo awali ndipo
tulimlaza mtoto kwenye kigodoro, alipoweka begi akakuta kuna blanketi.
“Alipolifunua akashtuka akasema
kuna nyoka watu wakaanza kukimbia ndani. Baadhi ya watu wenye roho yenye
hasira wakaamua kuingia ndani wakahakikishe kuna nini,” alisimulia.
“Walipoingia ndani ndipo wakakuta
ni mwili wa mtoto yaani marehemu. Waliposema ni mtoto wakipaza sauti
watu wakajaa ndani. Ndipo waumini wa yule mchungaji wakaanza kumpigia
simu yule mchungaji baadaye akarudi.”
Alisema baada ya mchungaji huyo kufika, aliingia ndani na waumini wake na kuanza kuomba.
“Walipoomba kwa muda mrefu ndipo
mchungaji huyo alipotoka nje na kushika MIC na kuuambia umati kuwa mtoto
baada ya kuombewa amehema mara mbili na ndipo watu wakaanza kulumbana,”
alieleza.
“Kama siyo mchungaji kuzusha yale
wala yasingekuzwa mpaka kwenye mitandao kiasi hiki. Sisi tunaamini
walioagizwa kuchukua mwili walichukua jeneza tupu pasipo kuwekwa mwili
ndani yake na kwa kuwa baada ya kutolewa jeneza hatukuingia ndani hivyo
tuliuacha mwili nyumbani tukaenda kuzika jeneza peke yake,” alibainisha.
Akizungumzia suala la imani ya familia
hiyo, Kyando alisema awali yeye na familia yake yenye watoto wawili,
walikuwa wakisali katika Kanisa Katoliki, lakini kutokana na matatizo ya
degedege yaliyokuwa yakimsumbua mwanawe wa kwanza, mkewe aliamua
kumpeleka mtoto huyo kwa mchungaji wa Kanisa la Bonde la Baraka ili
aombewe ikiwa ni sehemu ya kuhangaikia afya ya mtoto.
“Tulikuwa tunasali Roma, lakini
kutokana na matatizo ya mtoto, mama yake akaamua aanze kusali Kanisa la
Bonde la Baraka ili aombewe. Hapo mimi nikaacha kusali na ndiyo sababu
hata katika ibada ya maziko ya mtoto ikabidi tulishirikishe kanisa
walikokuwa wanasali mama na mtoto,” alisema Kyando na kuongeza:
“Watu wamezungumza maneno mengi
sana, siwezi kubisha japo ni ya uzushi ila wameongea kutokana na
walivyosikia, ila ukweli naujua mimi na namwachia Mungu.”
Naye baba mkubwa wa marehemu, Saulo
Kyando alisema jambo lililotokea lilikuwa la kawaida na kilichotokea ni
kukosekana kwa uratibu makini wa msiba huo.
“Hili jambo lilikuwa la kawaida
sema kilichokosekana ni mtu ambaye angeliweka jambo sawa, angekuwepo mtu
wa kusimamia kila hatua yasingefikia hapa,” alisema Saulo.