Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amezindua safari za ndege za Shirika la
Ndege Tanzania (ATCL) kutoka jijini Dar es Salaam kwenda Makao Makuu ya
Nchi, Dodoma.
Akizindua safari hizo leo amesema safari
hizo zitawezesha wafanyabiashara na wananchi wengine kutoka Dodoma na
kwenda katika maeneo mengine kwa urahisi.
“Tuna ndege nzuri. Tuzitumie kwenda
katika maeneo mengine kwani gharama zake ni nafuu. Kutoka Dodoma kwenda
Dar es Salaam ni sh. 165,000, kwenda na kurudi ni sh. 299,000,”
amesema.
Amesema ndege nyingine kama hiyo
inatarajia kuwasili nchini Juni mwaka huu jambo ambalo litaongeza idadi
ya safari za ndege hizo nchini na maeneo mengine ya nchi jirani.
Kwa upande wake Kaimu Mtendaji Mkuu wa
ATCL. Kapten Richard Shaidi ametumia fursa hiyo kuipongeza Serikali kwa
ujio wa ndege hizo na kwamba hiyo ni moja ya mikakati ya Mheshimiwa Rais
Dkt. Magufuli ya kufufua ATCL.
“Hivi karibuni tunaanza kwenda nchi
jirani. Mwakani tutapata ndege nyingine kubwa itakajayokuwa inafanya
safari za masafa ya kati na ya mbali” amesema.
Aidha, Mwenyekiti wa Bodi ya ATCL, Bw.
Emmanuel Korosso amesema hivi karibuni shirika hilo linatarajia kuanza
safari za kwenda katika miji ya Tabora, Songea, Mtwara, Mpanda, Mafia na
Jiji la Tanga.
Akizungumzia kuhusu safari za Dodoma
amesema zitafanyika mara mbili kwa wiki, siku ya Ijumaa na Jumatatu.
Hata hivyo wanatarajia kuongeza safari hapo baadae.
Naye Spika wa Bunge, Mheshimiwa Job Ndugai ametoa wito kwa wakazi wa
Dodoma kutumia vizuri fursa hiyo ya safari za ndege za ATCL kwa kuwa
utawawezesha kusafiri kwa muda mfupi tofauti na vyombo vingine vya
usafiri.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Bw. Jordan Rugimbana
ameshukuru kwa uanzishwaji wa safari hizo kwa kuwa zitarahisisha kutoka
katika Makao Makuu ya nchi na kwenda katika mikoa mingine nchini.