Mbeya Tena..Mwalimu Amvua Nguo Mwanafunzi na Kumtembeza Uchi Madarasani ili Azomewe na Wenzake..!!!


MIEZI michache imepita jamii haijasahau tukio la walimu wa sekondari ya Mbeya kumdhalilisha mwanafunzi, tukio linalokaribiana na hilo limetokea kwenye sekondari ya Ihanga jijini hapa kwa mwanafunzi wa kidato cha pili, Caleb Mwita kuchaniwa suruali na kutembezwa uchi madarasa yote akizomewa na wanafunzi.

Akisimulia tukio hilo jana, mzazi wa mwanafunzi huyo, Joseph Mwita wa Soweto jijijni hapa, alisema lilitokea mwishoni mwa wiki baada ya kijana huyo kuvaa suruali isiyotakiwa siku hiyo shuleni ndipo Mwalimu Mapunda alipomwadhibu kwa kumchapa viboko tisa.

Kama haitoshi, Mwalimu Bathlomew Kibona alimchania suruali hiyo ikidaiwa haiendani na sare za shule hivyo alimvua mwanafunzi viatu akaichana na kumwacha viungo vikionekana na kumtembeza madarasani kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne huku wanafunzi wa jinsi zote wakishuhudia.

Mkuu wa Shule, Theresia Mwaifwani alikiri kutokea kwa tukio hilo, lakini akasema Mratibu wa Elimu Kata ndiye mwenye jukumu la kulizungumzia.

Mratibu, Magdeni Sindika naye alikiri kuwapo tukio hilo na kusema mwanafunzi Caleb alikiuka kanuni za shule.

Aidha, Sindika alisema adhabu ya walimu hao ilikuwa kubwa kwa mujibu wa sheria na watajadiliana na Ofisa Elimu wa Jiji, ili kuona adhabu wanayostahili walimu hao na kumwomba mzazi awasamehe kwa walilofanya na kuahidi kumtafutia shule nyingine mwanafunzi huyo ili asome bila fadheha.

Mzazi Mwita alisema hapingi adhabu ya walimu hao lakini kitendo cha kuchaniwa suruali na kudhalilishwa kwa wanafunzi wenziwe hali na kumfanya kijana wake aathirike kisaikolojia hakikubaliki.

Caleb alisema suruali aliyovaa ni ya shule isipokuwa siku hiyo alivaa nyeusi badala ya kahawia na haikuwa inabana kama ilivyodaiwa na walimu na pia adhabu ya viboko ilitosha na si kuchaniwa suruali na kutembezwa madarasani akiwa uchi.  

Ofisa Elimu Taaluma wa Mkoa, Protas Mpogole alikiri kupata taarifa ya kutokea kwa tukio hilo na
kwamba Halmashauri ya Jiji Kitengo cha Elimu inashughulika suala hilo.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad