Rais wa Marekani Barack Obama amemtunuku makamu wake Joe Biden Medali ya Rais ya Uhuru, ambayo ndiyo nishani ya hadhi ya juu zaidi anayoweza kupewa raia nchini Marekani huku Biden, akionekana kushangazwa na hatua hiyo hali iliyosababishwa atokwe na machozi alipokuwa anatunukiwa medali hiyo.
Obama alimsifu Biden na kumwambia maneno haya, “Imani yako katika Wamarekani wenzako, kwa upendo wako kwa taifa na kwa utumishi maisha yako yote.”
Tuzo hiyo imetolewa kwa Bw Biden wakati wawili hao wanapojiandaa kuondoka madarakani Donald Trump wa Republican atakapoapishwa kuwa rais mpya tarehe 20 Januari. Bw Biden amesema anapanga kuendelea kushiriki siasa katika chama cha Democratic.
Joe Biden, aliyeonekana kutekwa sana na hisia, alisimama na kuonekana kushangaa Bw Obama alipomlimbikizia sifa na kumtaja kuwa “Chaguo bora zaidi, si kwangu tu, bali kwa Wamarekani”.
Medali hiyo ilikuwa na hadhi ya ziada, kwa mujibu wa gazeti la New York Times ambapo hadhi hiyo ya ziada, katika serikali za Marekani zilizotangulia, ilitunukiwa watu wachache sana, akiwemo Papa John Paul II.
Bw Obama alifanya mzaha kwamba mtandao sasa utakuwa na fursa ya mwisho ya kucheka na kufanyia mzaha kile ambacho kimekuwa kikiitwa “bromance”, maana yake upendo na urafiki wa dhati kati ya Obama na Biden.