SIKU mbili baada ya Baraza la Mitihani
la Taifa (Necta), kutangaza matokeo ya kidato cha pili na shule tisa za mkoa wa
Mtwara kushika mkia, Mkuu wa Mkoa huo, Halima Dendegu ameagiza mamlaka husika kuwavua
vyeo walimu wakuu wa shule za msingi 63 kutokana na matokeo hayo.
Akizungumza juzi Dendegu
alisema alichukua aumuzi huo baada ya kujiridhisha kutokana na utafiti ambao
waliufanya baada ya matokeo ya darasa la saba yaliyotoka mwaka jana.
Alisema taarifa zilizopo zinaonesha
wanafunzi hao wa kidato cha pili waliofeli walifanya vizuri kwenye matokeo ya
darasa la saba hali ambayo inaibua maswali mengi katika kufeli huko.
Mkuu huyo alisema zipo changamoto
mbalimbali ambazo zipo pia katika mikoa mingine ila Mtwara zimekuwa zikitumiwa
kama sababu za changamoto za mitihani.
“Hawa wanafunzi walifaulu mtihani wa
darasa la saba mwaka 2014/15 hivyo ni jambo la kushangaza kuona leo wanafeli,
lazima kuna uzembe kwa wasimamizi wa watoto hao katika ngazi ya msingi,”
alisema.
Alisema baada ya kuhoji baadhi ya walimu,
walidiriki kusema kuwa walitoa majibu kwa wanafunzi hao hali ambayo ilichangia
ufaulu, hivyo kusababisha kilichotokea.
Mkuu wa Mkoa alisema pamoja na walimu wakuu
hao kushushwa vyeo, bado wanaendelea na mkakati wa kubaini udhaifu wa walimu wa
sekondari na pia maofisa elimu ili wajiandae kuwajibika.
Dendegu alisema zipo changamoto kama
ufundishaji wa mazoea, kufanya mambo kwa kufupisha, utoro kwa wanafunzi, wazazi
kukosa mwamko na zingine nyingi.
Alisema pamoja na changamoto hizo, wana
mikakati ya kutoa chakula na kutaka maofisa elimu kufuatilia shule mbalimbali
lakini bado uzembe upo.