Mkuu wa Mkoa wa Arusha,Mrisho Gambo anatarajiwa kuwa Shahidi wa
kwanza katika kesi namba 351 ya mwaka jana inayomkabili Mbunge wa Arusha
Mjini, Godbless Lema na mke wake Neema Lema.
Mbele ya Hakimu Nestory Barro wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha,
katika kesi hiyo ya uchochezi Lema na mkewe wanadaiwa kutoa kauli za
kukashifu dhidi ya Gambo ambapo leo watuhumiwa hao wamesomewa hoja za
awali za shitaka linalowabili.
Lema alikuwa akitetewa na Wakili John Mallya na Sheck Mfinanga,huku Serikali ikiwakilishwa na Wakili Alice Mtenga.
Alice alidai Lema na mkewe walituma ujumbe mfupi wa sms, “Karibu
tutakudhibiti kama uarabuni wanavyodhibiti mashoga”, ujumbe unaodaiwa wa
kumuudhi na kumuumiza Gambo.
Baada ya kusomewa hoja hizo watuhumiwa hao walikana kutenda kosa hilo
ambapo pia Wakili Mallya alitoa notisi ya pingamizi la mdomo la
kuipinga hati ya mashitaka iliyowashitaki watuhumiwa hao kutokana na
kuwa na mapungufu ya kisheria na kuwa baadaye wataiomba Mahakama
iitupilie mbali hati hiyo.
Hakimu Barro aliahirisha kesi hiyo hadi Februari 3 mwaka huu,hoja za pingamizi hilo zitakapowasilishwa kwa njia ya mdomo.