Faru dume wanaoishi ndani ya Bonde la Ngorongoro mkoani Arusha wapo katika hatari ya kujeruhiwa au kuuawa na mtoto wa faru John aitwaye Telele.
Mmoja wa wahifadhi (jina tunalihifadhi) wa faru katika Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), alisema faru huyo amerithi tabia za baba yake za ukorofi, na tayari ni tishio kwa wenzake.
Faru John aliyefariki dunia usiku wa kuamkia Agosti 21, mwaka jana kutokana na uzee na maradhi, anatajwa kuwa mbabe kiasi cha kuwafukuza faru wengine kutoka Bonde la Ngorongoro na kuua wengine wawili kwa nyakati tofauti.
Kifo cha faru John kilizua utata mkubwa, kiasi cha Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kuagiza ufanyike uchunguzi wa kina ambao bado unaendelea.
Kwa mujibu wa mhifadhi huyo, ubabe wa faru John ulifikia hatua ya kupigana na baba yake aitwaye Rajabu kuanzia mwaka 2000 na baada ya vipigo mfululizo, Rajabu alihama kutoka Ngorongoro na kwenda eneo la Moru katika Hifadhi ya Taifa Serengeti ili kunusuru maisha yake.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopo Ngorongoro, faru John anatajwa kuwa faru mwenye umbo kubwa kuliko faru yoyote barani Afrika na mtoto wake Telele amechukua umbo la baba yake.
“Baada ya Rajabu kukimbia na kwenda Moru, Serengeti, walibaki madume watatu ambao ni John, Mikidadi na Runyoro, lakini kadri siku zilivyokuwa zikienda na ugomvi ulikuwa ukizidi, kila mmoja akitaka kuwa mkuu wa himaya, huku madume mengine yakiendelea kukua.
“Madume hayo ni pamoja na Msekwa, Telele, Ndugai na Selelii, na huyu Telele ana umbo kama la John na mkorofi sana.
“Mwaka 2003 mapigano yalizidi hadi pembe ya John ikakatika katika mojawapo ya matukio hayo ya kupigana, na baadaye Mikidadi na Runyoro nao walilazimika kukimbia, lakini baada ya kukatika, pembe hiyo ilianza kuota tena na kurudi kwenye makali yake.
“Baada ya madume hayo mawili kukimbia, mwaka 2012 faru John alimjeruhi kwa pembe mtoto wake mwingine aitwaye Cheusi… pembe ilipenya na kumchoma kwenye mapafu na maini na kumsababishia madhara makubwa,” alisema.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopo Ngorongoro, mwaka 2014 ilibidi pembe ya John ikatwe na mtaalamu kutoka Afrika Kusini, Peter Morkel, ambaye baada ya kuikata aliweka kifaa maalumu cha utambuzi (transmitter), ambacho kipo ndani ya mojawapo ya pembe alizokabidhiwa Waziri Mkuu Majaliwa usiku wa kuamkia Desemba 8, mwaka jana.
“Kuna wakati vikao vilipendekeza John apelekwe Afrika Kusini, lakini kutokana na historia yake ya ugomvi, wenzetu wa kule walikataa,” alisema mtoa taarifa.
TABIA NA MAISHA YA FARU
Kwa mujibu wa wahifadhi wa faru waliopo Ngorongoro na Serengeti, faru dume wana tabia ya kupigana kila mmoja akitaka kuwa mtawala wa wengine.
Mapigano ya faru wakati mwingine hudumu hata kwa zaidi ya saa tano na yanaweza kusababisha majeraha makubwa na hata kifo.
Ili kuwaachanisha faru wanaopigana, inabidi itafutwe gari na kuingia kati yao, na kwa kawaida baada ya kazi ya kuwaachanisha, gari huharibiwa vibaya na faru hao.
Pia faru jike akishapandwa, huchukua miezi 18 kuzaa, na kutokana na mazingira asilia mazuri kwa faru katika Bonde la Ngorongoro, anaweza kubeba mimba miezi sita baada ya kuzaa.
Hivi sasa kuna faru zaidi ya 50 Ngorongoro, kutoka faru 10 katika miaka ya 1980 hadi 1990, jambo linalotajwa kuwa limelotokana na juhudi kubwa na umakini katika uhifadhi wa mnyama huyo.