KIUNGO mshambuliaji wa zamani wa Yanga anayechezea Mbeya City, Mrisho
Ngassa amesema Yanga inahitaji wachezaji wawili wa kuchezesha timu ili
kuwa na uwiano mzuri.
Akizungumza Ngassa alisema Yanga inahitaji wachezaji wenye uwezo wa kuuchezea mpira na kutoa pasi za mwisho.
“Ukiangalia Yanga wanavyocheza kwa sasa, unaona kabisa inakosa watu
wa kuchezea mpira na kutoa pasi za mwisho kama alivyo Haruna Niyonzima
ili wawe na uwiano mzuri katika timu, lazima wawapate hao watu,”alisema
Ngassa.
Pia Ngassa alisema sababu hiyo ndio chanzo cha Yanga kufanya vibaya katika mchezo wa Kombe la Mapinduzi dhidi ya Simba.
“Mechi ilikuwa nzuri, Simba waliwazidi Yanga katikati kwani walikuwa
wanacheza mipira mirefu kumtumia Msuva peke yake, hivyo Simba wakagundua
njia hiyo, baada ya kusogea pembeni wakaua mipango ya Yanga,” alisema
Ngassa.
Ngassa alisema wachezaji wengi wa Yanga kwa sasa wamechoka baada ya
kucheza michezo mingi ya kimashindano, hivyo miili yao inahitaji
kupumzika.