MKUU wa Wilaya, Emmanuel Kipole, ameagiza
kukamatwa kwa Mtendaji wa Kijiji cha Luchili, Mathias Njolilo na Mwenyekiti wa
Kijiji hicho, Msazibwa Daud kwa tuhuma za kumtorosha Mchungaji wa Kanisa la
Agape anayetuhumiwa kunajisi mtoto wa miaka 13 (jina linahifadhiwa).
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi
ofisini kwake jana, Kipole alisema, haiwezekani Serikali ikemee vitendo vya ukatili
kama hivyo huku baadhi ya watumishi wakipokea fedha ili kuficha watuhumiwa.
"Nafuatilia tukio hilo, lakini kama
Mtendaji na Mwenyekiti wamemwacha mtuhumiwa,
naagiza vyombo vya usalama viwakamate na wamtafute aliko mtuhumiwa na watoe
maelezo kwa nini amemwacha huku akituhumiwa badala ya kumpeleka kwenye vyombo
husika," alisema Mkuu wa Wilaya.
Kauli hiyo ya Mkuu wa Wilaya ilikuja
baada ya mwandishi wa habari hizi kufuatilia tukio hilo kijijini na kuzungumza
na wananchi, huku Mchungaji naye akidaiwa kutoroka kijijini hapo, baada ya
kuachwa na viongozi wa kijiji wanaodaiwa kupokea fedha kutoka kwake.
Ilivyokuwa
Mchungaji huyo baada ya kumnajisi moto
huyo, alimsababishia maumivu makali sehemu zake za siri.
Tukio la kunajisiwa mtoto huyo lilitokea
Januari 10 nyumbani kwa Mchungaji huyo lakini licha ya kuomba msaada serikalini
ili akamatwe afikishwe kwenye vyombo vya sharia, hakuna hatua zilizochukuliwa.
Licha ya tukio hilo kufikishwa kwenye
ofisi ya Serikali ya Kijiji na mtuhumiwa kukamatwa na viongozi hao, aliachwa
katika mazingira ya kutatanisha yaliyojenga shaka kwa wananchi, na hajulikani
aliko.
Taarifa kutoka kijijini hapo zilieleza
kuwa baada ya kufanyiwa ukatili huo motto huyo alitoa taarifa ofisi ya Mtendaji
wa Kijiji na mtuhumiwa akakamatwa lakini aliachwa katika mazingira ya
kutatanisha.
Mmoja wa wakazi wa kijiji hicho, Asha
Hamud anayeishi jirani na Mchungaji huyo alidai kuwa siku ya tukio mtoto huyo
alionekana asubuhi akilia huku akionekana kuvimba mashavu na kutembea kwa
shida.
"Nilipomuuliza alisema amefanywa
vibaya na Mchungaji usiku kwa kumwingilia mara tatu na kumsababishia maumivu makali …
nilimchukua na kumpeleka ofisi ya Mtendaji wa Kijiji kuomba msaada ili mtuhumiwa
akamatwe," alidai mwananchi huyo na kuongeza:
"Baada ya muda Mtendaji wa Kijiji alimtuma
Mwenyekiti wa kitongoji cha Luchili Center, Msazibwa Daud ili akamkamate,
alimkamata na kumfikisha ofisini hapo na kumfungia kwenye chumba cha mahabusu
cha ofisi yake na kusubiri taratibu za kisheria".
Wakiwa wanasubiri taratibu hizo, baada
ya nusu saa zilichangwa fedha za nauli ili kumsafirisha mtoto huyo nyumbani
kwao mkoani Kagera, ili kupoteza ushahidi wa tukio na kwa taarifa
zilizopatikana, aliambiwa anapelekwa hospitalini kumbe alikuwa anasafirishwa.
Mtoto huyo alichukuliwa na Mwenyekiti wa
Kijiji, Daudi hadi Sengerema Mjini na kupandishwa basi la Bukoba, huku
akiambiwa anapelekwa hospitalini kwa uchunguzi wa afya yake.
Mtoto
asimulia
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi
akiwa mkoani Kagera mtoto huyo alidai kuwa Mchungaji huyo alimwomba kwa wazazi
wake kijijini Izibwa, Bukoba Vijijini kwa lengo la kumsomesha na siku ya nne
alipoulizia kuhusu shule Mchungaji alimjibu: "Shule utakwenda".
Ikiwa ni siku ya nne akiwa nyumbani kwa
Mchungaji huyo, alimlazimisha kufanya naye mapenzi huku akimshambulia kwa
kipigo.
Dada
aeleza
Dada wa mtoto huyo, Devotha Costantine
ambaye ni mtoto wa mama yake mdogo, alidai kuwa mdogo wake alifika kwake Kashai
mjini Bukoba akiwa na maumivu makali akilalamika kunajisiwa.
"Nilimwuliza kulikoni akasema amenajisiwa
na Mchungaji; wakati anamchukua alisema anakwenda kumsomesha, lakini
kilichotokea ni kunajisiwa, kitendo ambacho ni cha kikatili, tunaiomba Serikali
kumchukulia hatua Mchungaji huyo," alisema Devotha huku akibubujikwa na
machozi.
Alisema siku mdogo wake anafika,
alishangaa kumwona kwani hakumtarajia.
Kuhusu hali ya mdogo wake, alisema walimpeleka
kwenye matibabu na hali yake inaendelea vizuri.
Aidha, mmoja wa wananchi wa Luchili ambaye
hakutaka jina lake litajwe gezetini alisema siku moja baada ya tukio hilo,
Ofisi ya Mtendaji wa Kijiji hicho kupitia kwa Mtendaji wake, Mathias Njulilo
walituhumiwa kumwacha Mchungaji huyo kwa kupewa Sh 13,000.
Baada ya kumwacha baadhi ya wachungaji
wa madhehebu ya kikristo kijijini hapo, walimchangia nauli akatokomea pasipojulikana
na huku wananchi wakitupia lawama uongozi wa kijiji kukumbatia uovu kwa kupewa
fedha ili kuficha ukweli na kuomba Serikali iwachukulie hatua kali kisheria.
Mchungaji
Mchungaji anayetuhumiwa kumnajisi mtoto
huyo alizungumza kwa njia ya simu na gazeti hili akisema:
“Namwachia Mungu kwa kuwa ndiye muweza
wa yote na yote yanapatika kwa wanadamu, siwezi kusemea lolote juu ya suala
hilo limetokea, hata mimi sikutegema naomba msamaha msinitangaze manake ni
fedheha kwangu na wachungaji wenzangu aombaye msamaha kama ametenda kosa
husamehewa," alisema Mchungaji huyo.
Mtendaji
Mtendaji wa Kijiji, Njolilo alipoulizwa
kuhusu kumkamata mtuhumiwa na kumwacha, hakuwa tayari kuzungumzia suala hilo na
kusema hajui lolote licha ya Mwenyekiti wa Kjiji Ibrahimu Mbata kukiri kuwa alipewa
Sh 20,000 kama Mwenyekiti wa Kijiji wakiwa ofisini lakini akahoji alipewa za
nini na Mtendaji.