WIZARA ya Nishati na Madini imekanusha taarifa kwamba Waziri wake
Profesa Sospeter Muhongo katika kikao chake na Benki ya Dunia (WB)
kilichofanyika Septemba 28 mwaka jana kilijadilii mchakato wa kupandisha
bei ya umeme nchini.
Imeeleza katika taarifa yake kwamba katika kikao hicho walijadili
masuala ya upatikanaji wa umeme wa kutosha, uhakika na bei nafuu kwa
ajili ya kuchochea shughuli za maendeleo ya kukuza uchumi wa nchi ,
kuongeza ufanisi wa utendaji wa Shirika la Umeme (TANESCO) na kupunguza
deni la TANESCO.
Aidha katika taarifa kwa umma iliyotolewa jana na Wizara hiyo
ilieleza kuwa taarifa iliyotolewa na gazeti moja la kila siku kwa siku mbili mfululizo kuwa Waziri Muhongo alishiriki
katika kikao na ujumbe wa Benki ya Dunia kilichofanyika siku hiyo
kilichojadili kupandishwa kwa bei ya umeme, si ya kweli.
Wizara ilieleza kuwa wamekuwa wakifanya vikao na wadau mbalimbali
zikiwemo Taasisi za Umma, Binafsi na Washirika wa Maendeleo yakiwemo
Mashirika ya Kifedha ya Kimataifa kwa lengo la kuhamasisha uwekezaji
katika Sekta za Nishati na Madini nchini.
Taarifa hiyo ilifafanua kwamba siku hiyo ya Septemba 28 mwaka jana
kulifanyika kikao na ujumbe kutoka Benki ya Dunia ikiwa ni mwendelezo wa
vikao vya majadiliano kuhusu upatikanaji wa mkopo wa Dola za Marekani
milioni 200 kwa ajili ya kuboresha uendeshaji wa Shirika la Ugavi wa
Umeme (TANESCO).
Taarifa hiyo ilieleza kuwa kikao hicho pia kilihudhuriwa na taasisi
nyingine zikiwemo Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Shirika la Madini la
Taifa (STAMICO), Shirika la Maendeleo la Petroli Tanzania (TPDC),
Shirika la Maendeleo ya Taifa (NDC) na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na
Maji (EWURA).
Katika kikao hicho walijadili masuala ya upatikanaji wa umeme wa
kutosha, uhakika na bei nafuu kwa ajili ya kuchochea shughuli za
maendeleo ya kukuza uchumi wa nchi ikiwemo viwanda, biashara, kilimo na
huduma za jamii, kuongeza ufanisi wa utendaji wa Shirika la Umeme
(TANESCO) na Kupunguza deni la TANESCO.
Taarifa hiyo ya wizara ilieleza kuwa katika kulipunguza deni la
TANESCO ambalo linakaribia Sh bilioni 800 (takriban Dola za Marekani
milioni 363) na kuboresha shughuli za utendaji za TANESCO, Benki ya
Dunia ilijadiliana na Serikali ya Tanzania kupitia Wizara hiyo ili
kupata mkopo wa Dola za Marekani milioni 200.
“Hivyo, katika kikao hicho, hakukuwa na makubaliano ya kupandisha bei
ya Umeme kama ilivyoripotiwa na gazeti hilo,Vile vile, tunaomba
kuutaarifu Umma kwamba Wizara ya Nishati na Madini kwa niaba ya Serikali
inafanya majadiliano na Benki ya Maendeleo ya Africa (AfDB), Umoja wa
Ulaya (EU), JICA (Japan), na Mashirika mengine ya fedha kwa lengo la
kutafuta fedha za kuboresha Sekta ya Nishati,” ilisema sehemu ya taarifa
hiyo.