WAZIRI Mkuu wa zamani na Mjumbe wa Kamati ya Kuu ya Chadema,
Edward Lowassa, amemtaka Rais John Magufuli, kutafakari hoja na ukosoaji wa
wananchi na wapinzani dhidi yake.
Akizungumza katika Mkutano Mkuu Maalum wa Chadema wilayani
Misenyi mkoani Kagera uliyofanyika jana katika eneo la Bunazi, Lowassa alimtaka
Rais Magufuli kutozipuuza hoja zinazotolewa kuhusu masuala mbalimbali ya nchi.
“Tunamuomba Rais atafakari kwa ungwana hoja za watu
wengine. Tunamuheshimu ni Rais, lakini tunamuomba atafakari hoja hizi watu
wasiendelee kuumia sana,’’ alisema Lowassa.
Kuhusu na hali ya ukame nchini, Lowassa alisema kuwa hali
ya chakula nchini hivi sasa ni mbaya.
"Eneo moja ambalo hakika Rais anatakiwa kusikia hoja za
watu wengine ni suala la njaa. Nimeshuhudia mwenyewe pale Longido na maeneo
mengine. Hali ya mvua ni mbaya, hali ya chakula ni mbaya, watu wako hoi bin
taaban halafu wanaambiwa hakuna kuwapelekea chakula,” alionesha mshangao
Lowassa.
Akizungumzia madhila na waathirika wa tetemeko la ardhi
mkoani Kagera, Lowassa alielezea kushangazwa kwake na hatua ya Rais kuamua
kutopeleka misaada kwa waathirika hao akisema hata Mungu anashangaa.
"Mimi nakaa nasema mfano kama ni mama yako pale kijijini,
halafu amekumbwa na janga hili, anaambiwa ajisaidie mwenyewe si atakushangaa
hata Mungu atashangaa,’’ alisema kwa masikitiko.
Kwa upande wake Mbunge wa Bukoba Mjini, Wilfred Lwakatare
(Chadema), alisema hali ya chakula katika mkoa wa Kagera ni mbaya.
Lowassa akiambatana na wajumbe wengine wa Kamati Kuu ya Chadema,
akiwemo Profesa Mwesiga Baregu, ameendelea na ziara katikia mkoa wa Kagera ya
kuimarisha chama chao.