MJUMBE wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa ambaye pia ni
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan
amewataka viongozi wa CCM katika Mkoa Kaskazini (A) Unguja, kuwachukulia
hatua stahiki wanachama ambao wanakisaliti na kuhujumu shughuli za
kujenga CCM mpya.
Samia alitoa kauli hiyo wakati anafungua mafunzo maalum ya viongozi
na watendaji wa CCM na jumuiya zake wapatao 556 katika ngazi ya matawi,
wadi/tarafa na majimbo katika Mkoa wa Kaskazini (A) Unguja.
Alisema kuwa hatua hiyo itasaidia chama kuimarisha shughuli zake kwa
sababu kitakuwa na watu waadilifu na wenye nia ya kukisaidia kusonga
mbele na kupata ushindi mkubwa katika uchaguzi ujao.
Alisisitiza kuwa wanachama na viongozi wa CCM kote nchini waendelee
kuweka mipango na mikakati imara itakayowezesha chama kuendelea kupata
ushindi mkubwa na kushika dola.
Mjumbe huyo ambaye pia ni Mlezi wa CCM katika Mkoa wa Kaskazini A
Unguja alisema umoja na mshikamano miongoni mwa wananchama na viongozi
ndio silaha madhubuti itakayowezesha chama hicho kuimarisha shughuli
zake na kuongeza maradufu idadi ya wanachama nchini.
Alisema kwa sasa viongozi wanatakiwa kujielekeza katika kufufua na
kuimarisha jumuiya za chama ambazo katika baadhi ya maeneo hazifanyi
kazi vizuri ili zianze kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia kanuni na
taratibu za chama.