SERIKALI imewasilisha pendekezo la mabadiliko ya Sheria ya Bodi ya
Mikopo ya Elimu ya Juu ili kuwezesha wanafunzi wanaochukua Stashahada
katika vipaumbele vya kitaifa, kupewa mikopo ya kuwawezesha kuchukua
elimu husika.
Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa
Joyce Ndalichako alisema mabadiliko hayo, yamelenga kuwezesha kasi
katika uchumi wa viwanda.
Profesa Ndalichako alisema mabadiliko katika Sheria Namba 4 ya Mwaka
2016 ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), yamelenga
kutoa nafasi ya kada ya Stashahada inayohitajika ambao wamekuwa hawapati
mikopo.
“Kwa lengo la kupata balance (mizania) na kwa kuwa Diploma nayo iko
kwenye elimu ya juu, watoto ni wale wale. Kuna wengine nao wanashindwa
kumudu gharama na ili serikali ipate uwiano mzuri tumeona ni vizuri kuwe
na marekebisho ya sheria,” alieleza Profesa Ndalichako.
Profesa Ndalichako alisema kuna umuhimu mkubwa wa kada ya Stashahada,
hasa wanaokwenda sanjari na vipaumbele vya kitaifa kwenye msukumo wa
Serikali ya Awamu ya Tano wa ujenzi wa taifa la vijana, kama ilivyo kwa
wenye Shahada.
“Kama taifa tunazungumzia uchumi wa viwanda,wadau wote hata wale wa
ngazi ya kati ni muhimu katika kuhakikisha kwamba ajenda hii inafanikiwa
kama vile ambavyo wale wa digrii wangelifanya,” aliongeza waziri huyo.
Mwaka 2004, kulikuwepo na mabadiliko katika sheria hiyo iliyowezesha
wanaochukua masomo ya sayansi, hisabati na elimu ya msingi (kwenye
msisitizo wa sayansi na hisabati), kupata mikopo ya elimu, nafasi
iliyoanza kutumika mwaka 2014, lakini hatua hiyo ilisimamishwa wakati wa
muhula wa masomo wa mwaka 2016/17.
Hata hivyo, HESLB ilikaririwa ikisema kwamba maamuzi ya kusitisha
utoaji wa mikopo, ililenga kutekeleza maagizo ya serikali. Hata hivyo,
jana Profesa Ndalichako alisema kwamba uamuzi wa kusimamisha mikopo
hiyo,ulitokana na nia ya serikali kufanya mabadiliko katika sheria hiyo
ili kuipa wigo mpana zaidi kuliko kujikita katika eneo la sayansi pekee.
“Mwaka 2004 tuliingiza diploma, lakini kwa masomo ya sayansi pekee
sasa, tunataka kuwa na kipengele kinachopanua wigo ili tuweze kuhusisha
kozi nyingine za diploma ambazo zinaenda sanjari na vipaumbele vya
kitaifa,” alifafanua waziri huyo.
Kwa mwaka wa masomo 2016/17, serikali ilipanga bajeti ya Sh bilioni
483 ambazo zitakopeshwa kwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza na wale
wanaoendelea. Katika mwaka huo, wanafunzi wa mwaka wa kwanza waliopata
mikopo walikuwa ni 25,715.
Wakichangia mjadala huo, Mbunge wa Malindi, Ally Saleh (CUF)
alitahadharisha kuhusu vipaumbele vya kitaifa na kutaka kuwapo na
ufafanuzi ili kuondoa utata. “Sijafurahi sana na phrasing of national
priority.
Naogopa isije ikajibana au ikatumika katika hali itakayoleta utata.
Hivi karibuni tulikuwa na utata mkubwa wa nani apewe mikopo...sasa
tunasikia kuwa tunaenda kwenye uchumi wa viwanda isije fedha zote
zikapelekwa kule.
“Kutafutwe njia ya kudetermine hizo priority za kitaifa na kujua
watakuwa wangapi ili tujue kichumi itagharamu kiasi gani ilitusishindwe
huko mbele,” alisema Saleh.
Fikra ya kutanua wigo kwa wanafunzi wa Stashahada ilifafanuliwa na
watu wa Bodi ya Mikopo kwamba imezingatia kuwa katika sekta zote
kutatakiwa uwiano wa wataalamu wa kada mbalimbali. Aidha, imeelezwa kuwa
waziri kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, wataweza kushauriana na
kuona hitaji ya kada mbalimbali zinavyokwenda.