MAKAMU wa Rais Samia Suluhu Hassana ameishukuru Serikali ya India kwa ufadhili wake wa miradi ya maji katika miji 17 nchi ambayo inalenga kupunguza tatizo la maji kwa wananchi wengi nchini.
Samia alitoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam jana katika hafla ya Maadhimisho ya miaka 68 ya Siku ya Kitaifa ya Jamhuri ya India, iliyoambatana na uzinduzi rasmi wa majengo ya ofisi mpya ya Ubalozi wa India nchini.
Samia alisema ufadhili wa miradi ya maji na miradi mingine unaofanywa na Serikali ya India kwa Tanzania Bara na Zanzibar unadhihirisha wazi uhusiano mzuri uliopo ulioasisiwa na Mwalimu Juliu Nyerere na Mahatma Gandhi wa India.
Alisema kwa miaka mingi sasa uhusiano wa kindugu umekuwa ukiimarika katika sekta mbalimbali ikiwemo kisiasa, kidiplomasia, kibiashara, masuala ulinzi, utamaduni na mwingiliano wa watu na watu.
Aidha Makamu wa Rais pia aliishukuru Serikali ya India kwa msaada wake wa Sh milioni 500 alioutoa kwa wananchi wa Mkoa wa Kagera ambao walikumbwa na tetemeko la ardhi mwaka jana.
Katika hafla hiyo, Makamu wa Rais kwenye hotuba yake alitoa salamu za rambirambi kwa Serikali ya India kufuatia ajali ya treni iliyotokea katika Jimbo la Andhra Pradesh na kusababisha vifo vya watu 30 na kujeruhi wengine.
Kwa upande wake, Balozi wa India nchini Sandeep Arya alimhakikishia Makamu wa Rais Samia kuwa Serikali ya India itaendelea kudumisha na kuendeleza uhusiano mzuri uliopo kwa ajili ya manufaa ya wananchi wa pande zote mbili.