Shirikisho la Soka nchini
TFF limesema linasubiri maamuzi ya Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la
Mpira wa Miguu (CAF) kuhusu hatma ya timu ya taifa ya vijana ya
Serengeti Boys kufuzu ama kutofuzu michuano ya Afrika kwa vijana.
Hii
ni baada ya kukamilika kwa siku 10 walizopewa Shirikisho la Mpira wa
Miguu la Jamhuri ya Congo (FECOFOOT) kumpeleka mchezaji Langa Lesse
Bercy Cairo, nchini Misri kwa ajili ya kipimo kipya cha MRI.
Afisa habari wa TFF Alfred Lucas amesema, kamati ya utendaji ya CAF ilikaa kikao chake Januari 12 na kutoa nafasi ya mwisho kwa FECOFOOT kuhakikisha wanampeleka mchezaji Langa nchini Misri kwa ajili ya kipimo kipya cha MRI lakini mpaka jana ambayo ilikuwa ni mwisho mchezaji huyo alikuwa hajawasilki nchini humo hivyo wanaendelea kusubiri ili kujua maamuzi yatakayotolewa na CAF.
"Kwa mujibu wa kanuni za mashindano ya kimataifa ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 17, vijana waliohitajika kucheza ni wale wenye umri wa chini ya miaka 17," amesema Alfred.
Langa Lesse Bercy, amelalamikiwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwamba amezidi umri hivyo kuhitajika kumpeleka kwani hakustahili kucheza hatua ya kufuzu kwa michuano hiyo ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana.