MKUTANO wa Sita wa Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania unaanza leo mjini Dodoma. Serikali inatarajiwa kutoa kauli mbili kuhusu hali cha chakula nchini na deni la Taifa linaloenda sanjali na hali uchumi nchini.
Akizungumza na vyombo vya habari mjini Dodoma jana, Mkurugenzi wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano, Owen Mwandumbya alisema pamoja na kauli hizo za serikali, kabla yake kutakuwa na kauli ya Spika wa Bunge, Job Ndugai ambazo zitatolewa kabla ya kipindi cha maswali na majibu.
Katika kikao cha leo, kutakuwa na kiapo cha uaminifu wabunge watatu wa Kuteuliwa na mmoja wa kuchaguliwa ambao ni Abdallah Bulembo, Profesa Palamagamba Kabudi na Anne Kilango Malecela (wote wa Kuteuliwa) na mbunge wa kuchaguliwa kutoka Jimbo la Dimani Zanzibar, Ali Juma Ali (Dimani-CCM).
Katika mkutano huo, Kamati 14 za kisekta zitawasilisha taarifa mbalimbali ambazo zitajadiliwa na wabunge kadiri ratiba itakavyokuwa inaelekeza siku hiyo. Aidha, katika mkutano huo, itawasilishwa misaada mitatu.
Katika Mkutano wa Tano, miswada hiyo mitatu iliwasilishwa na ikasomwa kwa mara ya kwanza na baadaye ikapelekwa kwenye kamati sasa inaletwa bungeni kujadiliwa.
Miswada hiyo ni wa Muswada wa Sheria ya Madaktari, Madaktari wa Meno na Watalaamu wa Afya Wasaidizi wa Mwaka 2006, Muswada wa Huduma za Msaada wa Kisheria wa Mwaka 2016 na Muswada wa Marekebisho Mbalimbali ya Sheria Namba 4 wa Mwaka 2016.
Maswali 125 ya kawaida yataulizwa katika mkutano huo, ambao utamaliza shughuli zake Februari 10, mwaka huu. Pia katika mkutano huo, maswali ya Papo kwa Papo 16 yataulizwa kwa Waziri Mkuu.