BODI ya Utendaji ya Shirika la Fedha Duniani (IMF) imeeleza kuwa hali ya uchumi wa Tanzania ni nzuri.
Bodi hiyo imeeleza hayo baada ya kumaliza kufanya tathmini ya hali ya uchumi hapa nchini, chini ya Mradi wa miaka mitatu wa Kuwezesha Sera (PSI).
Katika taarifa yao iliyochapishwa katika tovuti, bodi ilisema kuwa ukuaji wa uchumi, ulikuwa vizuri katika nusu ya kwanza ya mwaka 2016 na hivyo kuleta matumaini ya kubaki katika ukuaji wa asilimia saba kwa mwaka huu wa fedha.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa bei za bidhaa zilishuka kufikia chini ya malengo ya asilimia tano. Hata hivyo, imetahadharisha kuwa kuna madhara ambayo yanaweza kuathiri ukuaji wa uchumi, ikiwemo msimamo mkali wa sasa juu ya sera zinazohusu uchumi mdogo.
Aidha, bodi imependekeza kuwa hali uchumi mdogo kwa sasa inapaswa kutafutiwa ufumbuzi, ikiwemo kulegeza msimamo katika sera za muda mfupi.
Hata hivyo, taarifa ya bodi hiyo inasema baada ya kupata ongezeko dogo kufikia Julai hadi Septemba, serikali ijizatiti kuongeza juhudi katika kutekeleza bajeti, na hasa katika uwekezaji wa kijamii.
Aidha imeeleza kuwa juhudi zilizofanywa na serikali katika kupambana na rushwa na ukwepaji wa kulipa kodi, zimesaidia kuweka msingi mzuri kwa kuongeza uwekezaji katika miundombinu kuanzia bajeti ya mwaka 2016/17.
Mradi wa PSI kwa kipindi kilichoishia Juni mwaka jana, umekuwa wa kuridhisha na malengo yote kufikia Septemba 2016 yalifikiwa.
Chanzo:Habarileo.