Shule yalia kuelemewa wanafunzi

SHULE ya Msingi Bunju `B' iliyopo Kata ya Mabwe Pande Manispaa ya Kinondoni, imeiomba serikali kujenga shule nyingine ili kuwe na shule mbili kutokana na shule hiyo kuzidiwa na idadi kubwa ya wanafunzi.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Angelina Rweyemera, alisema kwa sasa ina wanafunzi zaidi ya 2,060, idadi iliyovuka idadi ya wananfuzi wa wanaotakiwa kuwapo katika shule moja.

Rweyemera alisema kwa kawaida shule moja kuanzia darasa la kwanza hadi la saba, hutakiwa kuwa na wanafunzi 990, lakini shule yake ina idadi ya wanafunzi wa zaidi ya shule mbili.

Alisema kutokana na wingi wa wanafunzi katika shule hiyo, walimu wamekuwa katika wakati mgumu kufundisha.

"Tunaiomba serikali itujengee shule nyingine zipatikane shule mbili ili wingi wa wanafunzi tulionao sasa katika shule yetu upungue," alisema.

Rweyemera alisema hiyo itasaidia walimu kufundisha vizuri tofauti na ilivyo sasa.

Alisema licha ya shule hiyo hivi karibuni kujengewa vyumba viwili vya madarasa na Manispaa ya Kinondoni vilivyogharimu Sh. milioni 42 na kufanya kuwa na madarasa 18 huku ikipungukiwa na madarasa manne, bado wingi wa wanafunzi ni tatizo kubwa kwa walimu katika kumudu kuwafundisha vizuri.

"Shule ipo katika usalama mzuri kutokana na kuzungushiwa uzio na pia miundombinu ya maji na umeme ni mizuri, ila tatizo ni wingi wa wanafunzi ambao umepita kiasi, hivyo ikijengwa shule nyingine na wanafunzi wakapunguzwa, nina imani hali ya ufundishaji itakuwa bora katika shule yetu, " alisema Rweyemera.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad