Serikali kupitia
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imezitaka shule zote zilizowataka
wazazi/walezi kuwahamisha watoto wao kwa kigezo cha kutofikia wastani
wa ufaulu, kufuta agizo hilo na kuendelea na wanafunzi hao bila masharti
yoyote.
Taarifa
iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na Kaimu Kamishna wa Elimu,
Nicolas Buretta imeeleza kuwa wazazi wenye wanafunzi waliorudishwa
nyumbani kwa sababu hiyo wahakikishe wanawarudisha kwenye shule
walizokuwa wakisoma ili waendelee na masomo yao kama kawaida.
Kwa
mujibu wa taarifa hiyo, Serikali imefikia hatua hiyo baada ya kubainika
kuwa bado kuna shule nyingi za msingi na sekondari hususani zisizo za
Serikali na zaidi za kidini zinazoendelea kukaririsha, kuhamishia shule
nyingine au kuwafukuza wanafunzi kwa kigezo cha kutofikia alama za
ufaulu zilizowekwa na shule hizo jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
Badala
ya shule hizo kuchukua hatua hiyo, wizara hiyo imesema, “...Ziwe na
utaratibu wa kuinua viwango vya taaluma kwa wanafunzi wenye ufaulu mdogo
na hivyo siyo ruhusa kukaririsha darasa wanafunzi kwa kigezo cha
kutofikia wastani wa ufaulu uliowekwa na shule. Ikitokea, ni lazima
kufanya hivyo, taratibu zilizopo zifuatwe.”
Taarifa
hiyo imeelekeza wadhibiti ubora wa shule, kanda na wilaya, maofisa
elimu wa mikoa na wilaya kusimamia utekelezaji wa agizo hilo katika
maeneo yao.
“Shule yoyote itakayokiuka maagizo hayo itachukuliwa hatua kali kwa mujibu wa sheria zilizopo.”
Download Application ya Udaku Special Blog Kwa Kubonyeza Hapa