Jeshi la Polisi Mkoani Mwanza, linamshikilia Mkurugenzi wa kampuni binafsi iitwayo AQ Computer Co.Ltd na wenzake 7 kwa tuhuma za kukusanya fedha zaidi ya shilingi 100,000,000/= kutoka kwa wananchi kwa njia za udanganyifu.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza DCP Ahmad Msangi amesema mkurugenzi huyo anayefahamika kwa jina la Happy Aloyce Mbuya miaka 35 mkazi mtaa wa Ilemela, kwa kushirikiana na wenzake 7 kupitia taasisi ya AQ Power Club wamekuwa wakiendesha moja ya vikundi vinavyojihusisha na biashara ya upatu jijini Mwanza, inayotambulika kwa jina lisilo rasmi la kupanda mbegu na kuvuna.
Amesema upelelezi umebaini kuwa watuhumiwa hao wamekuwa wakiwashawishi wananchi kwa kuwadanganyana kuwarubuni wajiunge na biashara ya upatu ambapo wananchi hao hushawishiwa kuwekeza fedha kidogo kwa muda mfupi katika vikundi hivyo na baada ya hapo wanaahidiwa kulipwa fedha nyingi zaidi ya zile walizowekeza bila kufanya kazi yeyote.
Aidha Kamanda huyo wa Polisi mkoa wa Mwanza anatahadharisha wananchi kuhusu shughuli zinazofanywa na kikundi/ kampuni nyingine binafsi ya Bega kwa Bega Microfinance Company Ltd, kutokana na watu wengi kuripoti polisi juu ya kutapeliwa fedha zao na kampuni hiyo.
Taasisi nyingine aliyoitaja kufanya biashara hiyo ya upatu ni 'Amka Mwanamke' (AMWA) na kwamba uchunguzi unafanywa ili kuweza kubaini ukweli wa taarifa hizo.
Amesema tayari jeshi hilo limewatia mbaroni wakurugenzi na baadhi ya wafanyakazi wa kampuni hiyo na majalada ya kesi hizo yapo kwa mwanasheria wa serikali kwa hatua zaidi za kisheria.
Endapo tuhuma hizi zitathibitik, taasisi hizo ambazo ni AQ Power Club, Bega kwa Began a AMWA zitakuwa ni sawa na taasisi ya aina hiyo iliyojulikana kwa jina la DECI ya Jijini Dar es Salaam ambayo ilibainika kufanya utapeli wa njia hiyo mwaka 2008 na kuchukuliwa hatua za kisheria