KUNA kila dalili kwamba uamuzi wa Rais
John Magufuli kuwateua Profesa Palamagamba Kabudi na Abdallah Bulembo kuwa
wabunge, ni ishara ya kufanya mabadiliko katika Baraza la Mawaziri.
Hatua hiyo inatajwa kuchagizwa na
taaluma na uzoefu wa wateule hao na utendaji wa mawaziri takribani mwaka mmoja
tangu kuteuliwa kushika nyadhifa hizo.
Uchunguzi na maoni ya
wachambuzi wa masuala ya siasa nchini unabainisha, kwamba Rais Magufuli kimfumo
na matukio yanayoendelea nchini, yakiwemo yanayozikumba wizara, huenda akafanya
mabadiliko hayo ili kuendeleza kasi yake ya ‘Hapa Kazi Tu’.
Uteuzi wa Kabudi ambaye ni Profesa wa
Sheria wa Shule ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Bulembo
ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM, umefanya idadi ya wabunge
walioteuliwa na Rais Magufuli kufikia wanane, huku watano wakiteuliwa kuwa
mawaziri, mwingine Dk Tulia Ackson kuwa Naibu Spika wa Bunge.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu Dar es Salaam, Dk
Benson Bana alisema: “Siwezi kuwa mtabiri, lakini ukisoma alama za nyakati na
uteuzi huu kufanyika sasa, inawezekana si wote, lakini nafikiri anaweza (Rais
Magufuli) kufanya mabadiliko katika Baraza lake.
“Mfano Profesa Kabudi ni mzoefu, msomi
na anaijua Tanzania. Ana uwezo mkubwa, wa kujieleza na kujenga hoja. Sidhani
kama Rais atamwacha hivi hivi awe mbunge tu.”
Alisema Bulembo anaweza asiteuliwe kuwa
waziri, lakini akatumika bungeni kuimarisha umoja wa wabunge wa CCM.
“Huenda Magufuli anataka umoja wa CCM
usimamiwe vizuri. Binafsi naamini bado Lowassa (Edward) ana ushawishi miongoni
mwa wabunge wa CCM wa sasa. Bila kutafuta mbinu za kuhakikisha mizizi yake
inakatwa taratibu, italeta shida. Wanaangalia mwaka 2020 maana yeye (Lowassa)
ameanza kampeni mapema,” alisema Dk Bana.
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ya mwaka 1977 inampa Rais mamlaka ya kuteua wabunge wasiozidi 10 kutoka
miongoni mwa wananchi ambao anaona wanaweza kumsaidia katika utekelezaji wa
majukumu yake kwenye baadhi ya maeneo kama vile afya, elimu, kilimo, nishati na
sheria.
Ibara ya 66 (1) inasema, bila ya
kuathiri masharti mengine ya ibara hii, kutakuwa na aina zifuatazo za wabunge,
yaani (e) wabunge wasiozidi 10 walioteuliwa na Rais kutoka miongoni mwa watu
wenye sifa kwa mujibu wa ibara ya 67, isipokuwa sifa iliyotajwa katika ibara ya
67 (1) (b).
Walioteuliwa
Miongoni mwa wateule hao ni Naibu Spika,
Dk Tulia. Novemba mwaka juzi Naibu Mwanasheria Mkuu huyo wa zamani alichukua
fomu za kuwania uspika kupitia CCM kabla ya kujitoa dakika za lala salama, na
akateuliwa na Rais Magufuli kuwa Mbunge wa Viti Maalumu.
Baada ya kujitoa, alijitosa kuwania
unaibu spika ambapo wabunge 250 walimpigia kura ya ndiyo.
Wengine walioteuliwa kuwa wabunge na
kupewa wizara ni, Waziri wa Mambo ya Nje, Dk Augustino Mahiga, Profesa Makame
Mbarawa (Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano), Profesa Joyce Ndalichako (Elimu), Dk
Philip Mpango (Fedha) na Dk Abdallah Posi
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na
Watu wenye Ulemavu.
Rais Magufuli alipoteua Baraza la Mawaziri
Desemba 10 mwaka juzi, walikuwamo Dk Posi, Balozi Mahiga na Profesa Mbarawa
ambao waliteuliwa kwanza kuwa wabunge.
Wakati akitangaza Baraza hilo, alisema
aliacha viporo wizara nne za Maliasili na Utalii, Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Fedha na Mipango na Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, huku
akiteua naibu mawaziri kuongoza wizara hizo.
Desemba 23 alimalizia kiporo hicho kwa
kumteua Profesa Ndalichako na Dk Mpango kuwa mawaziri ikiwa ni baada ya kuwateua
kuwa wabunge.
Akizungumzia uteuzi huo, mhadhiri
mwingine wa UDSM, Richard Mbunda alitofautiana na Dk Bana na kusisitiza: “Kwa
kuzingatia utendaji wa mawaziri wenyewe na hali ilivyo sasa, sidhani kama kuna
sehemu (wizara) imelega. Unajua Magufuli wakati akiteua mawaziri alizingatia
sana weledi.
“Ndiyo maana Dk Mwakyembe (Harrison) yuko
Wizara ya Katiba na Sheria, hata Mahiga amebobea katika masuala ya uhusiano wa
kimataifa na yuko Wizara ya Mambo ya Nje. Huyu Makamba (Januari-Waziri Ofisi ya
Makamu wa Rais- Mazingira na Muungano), Shahada yake ya Uzamili amesomea
masuala ya utatuzi wa migogoro.”
Alisisitiza kuwa iwapo wizara kadhaa
zingekuwa zimetetereka, huenda uteuzi wa Profesa Kabudi ungeashiria kuwa
anakwenda kuziba pengo katika maeneo hayo.
“Nadhani anajaribu kuongeza idadi ya
wabunge bungeni maana nafasi 10 za uteuzi wa Rais huongeza nguvu ya CCM
bungeni. Sioni kama kuna kitu chochote kimemsukuma kufanya uteuzi huu,” alisema
Mbunda.
Rais Magufuli tangu alipotangaza kuunda
wizara 18 zenye mawaziri 19 na manaibu 16, huku sita kati yao wakiwa wanawake,
amefanya mabadiliko kwa kutengua uteuzi wa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani,
Charles Kitwanga na kumteua Mwigulu Nchemba aliyekuwa Waziri wa Kilimo na
Maendeleo ya Mifugo kushika wadhifa huo.
Kupitia mabadiliko hayo, Rais alimteua
Dk Charles Tizeba kuziba nafasi ya Mwigulu.
Katika mwaka mmoja wa utawala wake, Rais
Magufuli alimtosa waziri mmoja, kuhamisha mmoja na kuteua mmoja wakati
mtangulizi wake, Jakaya Kikwete alihamisha mawaziri 18.
Kikwete
Katika muhula wa pili wa utawala wake, Rais
Kikwete aliteua wabunge 10, kati yao sita aliwapa wizara za kuongoza, utaratibu
ambao Rais Magufuli aliutumia ili kupata mawaziri kulingana na mahitaji ya
Serikali yake.
Walioteuliwa na Kikwete kuwa wabunge na kupewa
wizara, ni Profesa Mbarawa, Shamsi Vuai Nahodha, Zakhia Meghji, Profesa
Sospeter Muhongo, Janet Mbene, Saada Mkuya na Asha-Rose Migiro. Alikamuilisha
orodha yake ya uteuzi wa wabunge 10 kwa kuwateua Dk Grace Puja na Innocent
Sebba ambao hakuwapa uwaziri.
Kabudi
Profesa Kabudi ambaye alipata kuwa Mkuu wa
Kitivo cha Sheria UDSM, alihitimu Shahada ya Sheria UDSM akipata daraja la
kwanza mwaka 1983 na Shahada ya Uzamili mwaka 1986 katika chuo hicho.
Alisoma Shahada ya Uzamivu ya Sheria ya
Chuo Kikuu cha Freie kilichoko Berlin, Ujerumani mwaka 1995. Profesa huyo pia
ni Msajili wa Kanisa la Anglikana Tanzania na pia alikuwa mjumbe wa Iliyokuwa
Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Bulembo
Bulembo ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya
Wazazi ya CCM tangu mwaka 2012, pia alipata kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Soka cha
Mkoa wa Mara (MRFA) na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka
Tanzania (TFF). Kwenye Kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka juzi, alikuwa Meneja wa
Kampeni wa Mgombea Urais wa CCM.