Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imesema haitaongeza siku za kufanya uhakiki wa namba ya utambulisho wa mlipakodi (TIN) hapa jijini baada ya muda kumalizika leo, hivyo wote watakaokuwa hawajahakikiwa watafutiwa namba zao na watatakiwa kuomba upya.
Kwa mara ya kwanza TRA imepanga kufanya uhakiki wa TIN kwa siku 60 kati ya Agosti na Oktoba lakini baada ya kujitokeza watu wengi tarehe ya mwisho iliongezwa hadi Novemba na mara ya tatu ilisogezwa hadi Januari 31. Lengo la uhakiki huo ni kuondokana na mfumo wa kizamani wa usajili wa namba hiyo.
Kayombo alisema kutokana na idadi kubwa ya watu waliokuwa wanahitaji kuhakikiwa namba, mamlaka iliamua kusogeza mbele muda wa kutoa huduma hiyo pamoja na kufungua vituo vya kutoa huduma ambako watumishi walifanya kazi hiyo hadi Jumamosi na Jumapili kuwapa nafasi wafanyakazi.
Alisema madhara kwa watakaofutiwa TIN ni makubwa kwani wafanyabiashara na madereva wa magari leseni zao zitakuwa batili na watachukuliwa hatua kwa kosa la kufanya biashara bila kuwa na namba ya utambulisho.
“Wale wote ambao watakuwa hawajahakikiwa watafutiwa namba zao za TIN, itawalazimu kuomba upya ingawa kuomba kwao upya hakutafuta madeni yao ya nyuma,” alisisitiza Kayombo.
Mmoja wa watu waliokwenda kuhakiki namba zao kituo cha Mwenge, Abdul Namwelesi alikosoa utaratibu huo akipendekeza uhakiki ungekuwa endelevu badala ya kuweka muda maalumu kutokana na ugumu wa watu wote kuhakikiwa kwa wakati mmoja.