Wakuu wa mashirika ya upelelezi nchini Marekani wanatarajiwa kukutana na Rais mteule wa nchi hiyo, Donald Trump na kumwonyesha ushahidi kuwa Urusi ilifanya jaribio lisilokifani kuvuruga uchaguzi wa Marekani kwa kufanya udukuzi katika chama cha wapinzani wake cha Democratic.
Mkutano huo unakuja wakati kukiwa na mvutano mkubwa kati ya viongozi wa mashirika ya ujasusi ya Marekani na rais huyo ajaye, ambaye anapinga vikali madai yoyote kuwa Urusi ilimsaidia kushinda uchaguzi wa rais.
Baada ya Trump kuonyesha wasiwasi kwa mara ya kwanza mapema mwezi uliopita, Rais Barack Obama aliyaamuru mashirika ya upelelezi kutoa ripoti ya kina kuhusu mashambulizi ya mtandaoni na uingiliaji wa Urusi katika uchaguzi wa rais.
Obama alifahamishwa kuhusu ripoti hiyo jana na wakuu wa ujasusi na wanatarajiwa kuzungumza na Trump hii leo.