SHIRIKISHO la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta), limeahidi
kutangaza kwa serikali mapendekezo yake ya kima cha chini cha mishahara
kwa watumishi wa umma na sekta binafsi wakati wowote kuanzia sasa.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Rais wa Tucta, Tumaini
Nyamghokya, mapendekezo hayo ya kima cha chini na nyongeza ya mishahara
yanaendelea kufanyiwa kazi na wataalamu wao.
“Tunataka mapendekezo hayo mapya yamfikie Rais John Magufuli mapema
kabla ya maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani, Mei Mosi,” alisema
Nyamghokya.
Nyamghokya aliyasema hayo juzi alipokuwa akifungua Mkutano Mkuu wa
Kanda ya Nyanda za Juu Kusini wa Chama cha Wafanyakazi wa Viwanda,
Biashara, Taasisi za Fedha, Huduma na Ushauri (TUICO).
Alisema baada ya mapendekezo hayo kutoka, Tucta itazungumza na
kiongozi huyo wa nchi ili kuyatetea kwa kuwa yanalenga kuongeza motisha
kwa wafanyakazi nchini.
Alisema kwa jinsi hali ilivyo hivi sasa (hakuitaja hali hiyo) wana
matarajio Rais atayachukua mapendekezo yao na kuyafanyia kazi. Pamoja na
mapendekezo hayo, kiongozi huyo wa Tucta alisema wafanyakazi
wanaelemewa na mzigo mkubwa wa kodi zinazokatwa katika mishahara yao.
“Kodi hizo zimeleta manung’uniko kwa watumishi hasa wenye mishahara
ya kima cha kati na cha juu kwa kuwa makato yao ni makubwa,” alisema.
Alisema Tucta inataka Rais awatetee wafanyakazi kama alivyoonesha
kuwatetea wafanyabiashara ndogo (machinga) waliotaka kuondolewa na
mamlaka katika maeneo yao bila kuoneshwa maeneo mapya ya kwenda. Alisema
wafanyakazi wanaunga mkono juhudi mbalimbali zinazofanywa na Rais
katika kushughulikia changamoto za nchi.