Habari za leo wapendwa wasomaji wa safu yetu hii inayozidi kujizolea
umaarufu. Ni imani yangu kuwa mambo yanakwenda sawa na kila mmoja wenu
anaelewa kuhusu mada mbalimbali ninazowaletea.
Mara nyingi nimekuwa nikizungumza zaidi kuhusu wanawake wenzangu,
lakini leo nimeona acha niwageukie akina baba kidogo, kwa sababu yale
yote tunayoelekezana kila siku yanalenga kuimarisha ndoa na uhusiano
wetu, ambao wanaoubeba ndiyo hawa wenza wetu tunaopenda kuwaita kichwa
cha nyumba.
Hapa nizungumzie kuhusu uhusiano. Tunatambua kuwa huwezi kuwa mke au
mume bila kwanza kuanza na mwenzi wako katika urafiki, uchumba na
hatimaye ndoa. Lakini ukiangalia maisha ya sasa, hasa mijini, kati ya
wanaoishi chumba kimoja, kwa maana ya kupika na kupakua zaidi ya
asilimia 75 ni ambao hawajaoana.
Yaani wanaishi kwa miaka mingi kama marafiki tu, kisingizio kikubwa
cha kinababa wengi ni kuwa hawajajipanga, eti wakiwa tayari watafunga
ndoa, kana kwamba kuoa kunahitaji mamilioni ya shilingi.
Akina baba wengi wamekuwa wakijifikiria wao tu, kwani ni ngumu kwao
kujua kuwa kadiri penzi
linavyochukua muda mrefu ndivyo pia umri
unavyozidi kuwa mkubwa na kwetu sisi wanawake, tunavyokua wakubwa kiumri
ndivyo uzuri wetu nao unapungua.
Hivi, kama kweli unampenda mpenzi wako na mko pamoja kwa miaka kibao,
kuna tatizo gani kumuoa? Huoni kama kwa kukaa kwako kimya kwa muda
mrefu unamkosesha mwenzio bahati yake?
Lakini hata hivyo, tatizo la wanaume kukaa muda mrefu na wanawake bila kuwaoa linachangiwa kwa kiasi kikubwa na sisi wanawake wenyewe. Tuko rahisi sana kukubali kusubiri bila kujua kuwa kadiri tunavyoendelea, ndivyo na thamani yetu kama akina dada inaisha.
Inavyoonekana, hatujui kama kuna hasara ya kuendelea kusubiri ndoa.
Ukiwa na mwanaume kwa muda mrefu ni rahisi kukuchoka, hasa kama mtakuwa
na migogoro. Hapo unampa kisingizio cha kukuacha kwa kile wanachosema,
eti labda baada ya kukupima anakuona hufai.
Wakati mwingine hiyo hutokea anapokuwa amepata kimada huko pembeni
ambacho kikiwa makini anaweza kumuoa na wewe kuendelea kuwa kimada
mzoefu.
Pia wanawake tuna tatizo la uvumilivu kupita kiasi na wepesi
kusamehe, ndiyo maana tunakubali kukaa na maumivu ya kutoolewa kwa
kipindi kirefu bila kuelewa jambo hilo linatumiwa na wanaume kutuadhibu.
Ninachowaomba wanaume, ni kuweka imani yao ya kidini mbele, wawe na
muda mfupi na wenza wao ili waamue kama ni kufunga nao ndoa au la ili
kuwapa nafasi ya kufanya mambo mengine.
Kaa na ujiulize utajipanga mpaka lini, lakini pia kama unampenda kwa dhati mpe nafasi auone upendo wako kwa kumuoa.