Tukio la mwanamke mmoja mkoani
Mara kucharazwa viboko 50 na wanaume wanaodaiwa ni wa kutoka kwenye
baraza la kimila, ndilo lililofunga mwaka 2016 na kuufungua mwaka mpya
wa 2017, lakini Uwazi limekuwa gazeti la kwanza kuzungumza na
mwanamke huyo ana kwa ana ambaye amesimulia mazito juu ya nini
kilitokea, kubwa zaidi ni ujauzito wake kuharibika kwa sababu ya kipigo.
TUJIKUMBUSHE KWANZA
Januari 9, mwaka huu, video
inayomwonesha mwanamke huyo akiwa anacharazwa viboko na wanaume
wasiopungua wanne ilisambaa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii kiasi
cha kuzua taharuki katika jamii.
Wengi walilaani tukio hilo huku habari
zikisema kuwa, Polisi Makao Makuu jijini hapa walitoa agizo kwa
makamanda wote wa polisi wa mikoa nchini kufuatilia kwa kina tukio hilo
la kinyama ili kubaini lilitokea wapi baada ya video hiyo kutotoa
ushirikiano wa sehemu husika.
JANUARI 12, 2017
Januari 12, vyombo vya habari vikaripoti
kuwa, tukio hilo lilitokea wilayani Rorya, Mkoa wa Mara ambapo watu
kumi walikamatwa wakihusishwa na tukio hilo lililotafsiriwa kuwa ni la
kudhalilisha na kuondoa utu wake.
UWAZI LAFUATILIA KWA KINA
Kwa kawaida, kukamatwa kwa watu hao kumi
na kufikishwa kwenye Kituo cha Polisi cha Rorya ilikuwa ndiyo hitimisho
la tukio hilo licha ya kwamba, Watanzania walio wengi walikuwa na kiu
ya kujua kisa cha tukio na mhusika anasemaje na nini kinandelea? Ndipo
Gazeti la Uwazi, kama kawaida yake ya ufuatiliaji wa matukio hata ndanindani, lilijivika jukumu la kufuatilia.
JANUARI 14, 2017
Januari 14, mwaka huu katika Kitongoji cha Kwitonyi, Kijiji cha Kinesi, Kata ya Nyamuga, Wilaya ya Rorya mkoani hapa, Uwazi
lilikutana ana kwa ana na Ghati Chacha Makori (32) ambaye alikiri kuwa,
yeye ndiye yule mwanamke anayeonekana kwenye video akicharazwa viboko.
UWAZI LAMKUTA AMEKAA UPANDEUPANDE
Nje ya nyumba yake ya matofali ya
kuchoma, Ghati alikuwa amekaa upandeupande na alipoulizwa alisema kuwa,
mpaka siku hiyo ya Jumamosi alikuwa anasikia maumivu makali sana
yaliyotokana na kupigwa viboko hivyo hakuwa anaweza kukaa kwa makalio.
HII HAPA SIMULIZI YAKE
Akizungumza na Uwazi nyumbani hapo, Ghati, mama wa watoto wanne, alisema:
“Ilikuwa Desemba 23, 2016, majira ya
kama saa 2:00 hivi asubuhi, mimi nikiwa hapa nyumbani kwangu na familia
yangu, walifika vijana wawili, pia ni wakazi wa kijiji hiki, wakaniambia
naitwa na wazee wa kimila wa kijiji.
“Mimi niliwaambia wale vijana kwamba,
sitaweza kwenda huko kwa sababu naumwa, na kweli naumwa hata sasa.
Lakini cha ajabu, wale vijana waligoma kuondoka kupeleka majibu,
wakaamua kunibeba kwa nguvu kwenye baiskeli hadi kwa wazee wa kimila
ambao niliwakuta wamekusanyika kwenye mkutano chini ya mti.
WAZEE WAMHUKUMU
“Baada ya kufikishwa kwenye mkutano huo
wa kimila, wale wazee wa kimila walinihukumu kwa kuamuru nichapwe viboko
hamsini (50) bila kunieleza kosa langu ni nini! Wala hawakunipa nafasi
ya kujieleza kwenye mkutano huo uliokuwa ukiongozwa na wazee 12.
UJAUZITO WA MIEZI MITATU WAHARIBIKA
“Nikiwa nashangaa sasa, ghafla walianza
kunicharaza viboko kwenye makalio huku wakiwa wamenilaza chini na
kunikanyaga shingoni ili nisitapetape.
“Hali ile ilinisababishia maumivu makali
sana. Kwa kweli maumivu yalikuwa makali sana. Mbaya zaidi wakawa
wanaitana kuja kunicharaza viboko. Kila mmoja alichapa idadi yake.
“Nilikuja kushtuka nikiwa navuja damu nyingi. Nilikuwa na ujauzito wa miezi mitatu nao ukachoropoka.
AELEZWA KISA CHA KUCHARAZWA VIBOKO
“Baada ya kuchapwa viboko hivyo, wale
wazee walimuita mbele yangu mama yangu mzazi, anaitwa Anna na kisha
wazee hao wakanieleza mbele ya mama kwamba, wamenicharaza viboko kwa
sababu mama yangu aliwapelekea malalamiko kwamba, nimemtukana na kumuita
mchawi na kumkana kuwa yeye si mama yangu mzazi na kwamba nitamuua kwa
sumu kwa vile amekatalia nisiuze matofali yangu.”
MADAI YANA UKWELI?
“Ni kweli yule ni mama yangu aliyenizaa,
lakini namkataa kabisa kuwa si mama yangu kwa sababu alinifanyia unyama
mkubwa bila kujali kuwa mimi ni mtoto wake wa kwanza wa kuzaa na kwa
sasa nina mji (makazi) wangu.
“Kisa kiko hivi, nilifyatua matofali
5,800 nyumbani kwetu anapoishi mama, nikayachoma ili niyauze, nilipe
mkopo wa watu, lakini mama aliyakatalia matofali hayo nisiyauze, hivyo
mimi sioni sababu ya kumuita mama yangu. Mimi najua alipoona nakazania
kuuza matofali yangu akaamua kunisemea kwa wazee wa kimila ili nichapwe
viboko kama njia ya kunitisha,” alisema Ghati kwa sauti ya kujiamini.
MAMA WA GHATI ANASEMAJE?
Baada ya kusikia maelezo ya Ghati, Uwazi
lilimfuata mama yake, Anna Chacha Makori (53), ambaye katika utetezi
wake wa kwa nini alimfikisha bintiye kwa wazee wa kimila, alisema:
“Mimi niliamua kumpeleka Ghati kwa wazee
wa kimila ili apigwe viboko kwa sababu ananidharau na kuanza kunitukana
kuwa mimi ni mchawi mkubwa na kwamba ataniua. Pia amenikana kwamba mimi
sijamzaa.”
BARAZA LA WAZEE WA KIMILA LAFUTWA
Matiku Wambura Iramba ni Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Kinesi, yeye akizungumzia tukio hilo alisema:
“Ofisi yangu imepokea kwa masikitiko
makubwa taarifa za kuchapwa viboko kwa Ghati kwani baraza hilo la kimila
lilikuwa likifanya shughuli zake kinyume cha sheria bila ofisi yangu
kuelewa. Desemba 21, 2016 (siku mbili kabla ya tukio la Ghati) ofisi
yangu ililiandikia baraza hilo barua rasmi ya kulifuta baada ya
kulalamikiwa na wananchi juu ya utendaji kazi wake unaokiuka haki za
binadamu.
“Kwa hiyo ninachoweza kusema ni kwamba,
tayari baraza hilo nimelifuta. Sijui tena wazee hao walikaa na
kuendesha vikao vyao kwa kibali cha nani, nasubiri huyo mwathirika wa
tukio alete barua za hospitali ili niwachukulie hatua kali wale wote
walioendesha zoezi hilo la kinyama.”
SHUGHULI ZA GHATI
Ghati alisema amekuwa akipata riziki
yake ya kila siku kwa kufanya shughuli za kilimo cha bustani ya
mbogamboga lakini kwa sasa hawezi kwenda bustanini na hivyo kutegemea
msaada wa watoto wake wadogo.
KAULI YA KAMANDA WA POLISI KANDA
MAALUMU akizungumza na gazeti hili Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalum
ya Tarime, Rorya ACP Sweetybert Njewike alisema wamemtafuta Ghati
lakini wameshindwa kumpata kwa kuwa wazee wa Kimila wamemficha.
Kama kuna uwezekano wa kumleta hapa
kituoni mleteni wale wazee wamemficha baada ya kumfanyia ukatili ule”,
alisema na kuongezakwamba tabia ile ya kimila haifai na inapaswa kupigwa
vita na kila Mtanzania.
Shenzi type na mila zenu zilizopitwa na wakati kwani hii siyo miaka ya 1605 mila gani hizo za kishenzi za kumgandamiza mwanamke kama vile mtumwa?Hii ni karne nyingine kila binadamu ana haki sawa na mwingine bila kujali jinsia yake hii ni kwenu nyote mliokuwa na fikra hizi za kishenzi za miaka hiyo ya stone age mlaaniwe
ReplyDeleteYaani huyo mama yake mzazi ni katili wa hali ya juu yaani alikuwa hapo wakati mwanae akipigwa namna hiyo, kweli ni heri ulimkana kuwa siyo mama yako mzazi maana hastaili kuitwa mama, mimi mwenyewe mama yangu ni katili namna hiyo nilichokifanya ni kuhama mbali na kukata mawasiliano sababu mama yangu mzazi alitaka kuniua aliniwekea sumu kwenye chakula bahati nzuri niliwahi kwenda hospitali nikatibiwa nikapona, tangia hapo mama haji tena kuniona katika maisha yangu yote nitakayoishi, kuna wazazi makatili sio wazazi wote wanawapenda watoto wao, hao waliokamatwa kufanya ukatili huo serikali iwachukulie hatua kali na mama mtu akamatwe pia ndiyo yeye kasababisha mwanae achapwe na mama yake achukuliwe hatua kali za kisheria sababu wamesababisha mwanamke wa watu mimba yake itoke na vile vile angeweza kupoteza maisha kwa kuchapwa namna ile.
ReplyDeleteKatika maisha yangu sijawahi kuona ukatili kwa mwanamke katika kiwango hicho.Mama mzazi alimpeleka mtoto wake kwa wazee wa mila kupata adhabu kisa mama hataki matofali aliyoatengeneza mtoto wake wa kike yauzwe. Mtoto ana kosa gani hapo?
ReplyDeleteSIJAONA UKATILI KAMA HUU
ReplyDelete