MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imemwachia huru Mfanyabiashara Juma
Mwinyi maarufu ‘Neti’ aliyekuwa akidaiwa kumweka reheni mdogo wake
nchini Pakistani kwa Sh bilioni 1.5.
Uamuzi huo wa mahakama umetolewa mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi,
Cyprian Mkeha baada ya kupitia hoja mbalimbali za kisheria na
kujiridhisha kwamba mshtakiwa alikamatwa bila kufuata utaratibu.
Juma aliachiwa huru ikiwa ni miezi minne tangu kufikishwa mahakamani
hapo kwa mara ya kwanza akishtakiwa kwa kosa la kusafirisha binadamu
kwani alishtakiwa Agosti 3, mwaka jana na aliachiwa huru Desemba 19,
2016.
Awali akisoma mashtaka Wakili wa Serikali Mkuu, Peter Njike alidai
kati ya Desemba Mosi mwaka 2015 na Julai 15 mwaka 2016 jijini Dar es
Salaam mshtakiwa alitenda kosa la kusafirisha binadamu kinyume cha
sheria.
Njike alidai Juma alijifanya anakwenda kumpa mafunzo Adam Akida Mkazi
wa Magomeni, Mtaa wa Chemchem na Idrisa na badala yake alimsafirisha
kwenda nchini Pakistan kwa ajili ya kumweka reheni.
Mshtakiwa alifikishwa kwa mara ya kwanza mahakamani hapo Agosti mwaka
jana na kufunguliwa kesi namba 276/2016 ambayo ilifutwa Novemba 11,
mwaka jana kwa kutumia kifungu cha sheria namba 225 (5) cha Mwenendo wa
Makosa ya Jinai na kukamatwa tena.
Juma alikuwa chini ya mikono ya Polisi tangu alipokamatwa tena
Novemba 1, mwaka jana hadi Novemba 14 ambapo alishtakiwa tena kwa
mashtaka haya hayo katika kesi namba 411 ya mwaka 2016.
Wakili wa mshtakiwa huyo Hudson Ndusyep, aliwasilisha hoja mahakamani
hapo Desemba 7, mwaka jana akidai mteja wake ameshtakiwa kimakosa kwa
sababu sheria za ukamataji zimekiukwa kwani alikamatwa bila kuwepo kwa
hati ya kumkamata, hivyo aliomba kesi ifutwe mshtakiwa aachiwe huru.
Akijibu hoja hizo Wakili wa Serikali Mwandamizi, Hellen Mosha,
alipinga hoja za utetezi na kuiomba mahakama isimwachie huru mshtakiwa
na kwamba hoja ya hati ya kumkamata itaangaliwa wakati kesi inaendelea
na hoja za utetezi haziko katika msingi wa kisheria.
Akisoma uamuzi Desemba 19 mwaka jana baada ya kusikiliza hoja hizo
Hakimu Mkeha alisema mshtakiwa alishtakiwa kwa kosa la kusafirisha
binadamu chini ya kifungu namba 4(1)(a)na (5) cha Sheria ya Kuzuia
Usafirishaji Binadamu namba 6 ya mwaka 2008.
Katika sheria hiyo kifungu namba 12 (1) kinasema wazi kwamba polisi
hawezi kukamata mtu kwa kosa lolote lilipo chini ya sheria hiyo bila
kuwa na kibali cha kukamata, hivyo mahakama ilikubaliana na hoja za
utetezi kwamba utaratibu wa kumkamata mtuhumiwa ulikiukwa.
“Kwa mujibu wa sheria hakuna njia nyingine zaidi ya kuondoa mashtaka dhidi ya mshtakiwa na kumwachia huru mshtakiwa.
“Naushauri upande wa mashtaka wakati wowote wanapofuata taratibu za
ukamataji wamfikishe mshtakiwa mahakamani,” alisema Hakimu Mkeha.
Mwanzo wa sakata la Juma
Hatua ya kukamatwa kwa Juma, ni matokeo ya gazeti hili kuripoti
habari za Mtanzania kushikiliwa ughaibuni kutokana na biashara ya dawa
za kulevya Julai 18, mwaka jana.
Habari hizo ziliripotiwa baada ya kipande cha video kusambaa katika
mitandao ya kijamii Julai 17, mwaka jana ikimwonesha Adamu Akida
amewekwa chini ya ulinzi na maharamia hao wenye silaha.
Gazeti la MTANZANIA lilifuatilia tukio hilo na kubaini kuwa Adamu alikuwa
amewekwa rehani kwa gharama ya Sh bilioni 1.5 kwa kile kilichoelezwa
kuwa ilikuwa ni utekelezaji wa mpango wa biashara ya ‘unga’.
Kutokana na hatua hiyo, timu ya Gazeti la MTANZANIA iliamua kuchimbua suala
hilo ili kujua ukweli wa namna kijana Adamu Akida, alivyokuwa kwenye
mateso hayo.
Akisimulia tukio hilo kaka yake aliyejitambulisha kwa jina la Hemed
Abdallah (si jina lake halisi) alisema, Adamu alikwenda kwa kaka yake
ambaye ni mtoto wa mama yake mdogo aliyetambulika kwa jina la Juma na
kuomba msaada wa mtaji kwani kazi yake ya kinyozi haikuwa ikilipa na
hali ya maisha ilikuwa ngumu.
Alisema baada ya kueleza shida yake, Juma alimuhoji kama yupo tayari
kwa ajili ya kutafuta maisha nje ya nchi na Adamu alikubali kufanya kazi
ya aina yoyote ili mradi aweze kupata fedha.
“Awali alikwenda kwa kaka yake mtoto wa mama yake mdogo anaitwa Juma
na kuomba asaidiwe mtaji kwani amekuwa na maisha magumu sana. Baada ya
hali hiyo aliambiwa kuna safari ya kwenda Pakistan ambayo waliondoka
wakiwa wameandamana watu watatu pamoja na Juma na kijana mwengine ambaye
jina lake limenitoka, ila anaishi Kinondoni.
“Walipofika kule, Juma akachukua mzigo akiwa na yule kijana wa
Kinondoni, huku Adamu akiachwa Pakistan kwa maelezo kuwa baada ya siku
tano atakuja nchini na mzigo mwingine. Muda wote hata tukihoji alipo
Adamu tunaambiwa yupo anaendelea na kazi huko aliko na angerudi mwezi wa
tisa au wa nane.
“Sasa hii video ndiyo imetupa picha halisi ya Adamu, maskini sijui
kama tutampata akiwa hai. Hata hivyo kwa kipindi cha hivi karibuni,
tulikuwa tukishangazwa na mwenendo wa Juma kwani amekuwa na fedha nyingi
sana hadi kufikia kuwajengea nyumba dada zake pamoja na kuwanunulia
magari,” alisema Abdallah huku akibubujikwa na machozi.
Mke alivyohama
Julai 19, mwaka jana chanzo cha uhakika kilisema kuwa mke wa Adamu ambaye alikuwa akiishi Mtaa wa Sunna, Magomeni, alihamia Kijitonyama.
Mke huyo wa Adamu, alihamishwa na shemeji yake, Juma ambaye ndiye aliyempangia nyumba nyingine Kijitonyama.
Kauli ya Mwenyekiti wa Mtaa
Akizungumza na Mtanzania, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Idrissa,
Issa Mpangile, alisema askari kutoka makao makuu ya Jeshi la Polisi
walifika katika ofisi yake na kumtaka waongozane kwenda katika nyumba ya
baba mdogo wa Adamu.
Alisema walipofika nyumbani kwa Kessy Baharia Mtaa wa Idisa, ambaye
ndiye baba mdogo wa Adamu, polisi walichukua maelezo yake na baadaye
wakarudi katika ofisi ya Serikali ya Mtaa kuchukua maelezo yake.
Akizungumzia kuhusu kijana huyo, Mpangile alisema kuwa ni mzaliwa wa mtaa huo, lakini baadaye alihamia Mtaa wa Suna ambao ni jirani na Mtaa wa Idrissa, Kata ya Magomeni.
Alisema wakati kijana huyo anahama mtaa huo, alikuwa bado ni kinyozi na hakuwa na rekodi ya kusafiri kwenda nje ya nchi.
Alisema katika mazungumzo na Baharia, alimweleza kuwa amewasiliana na baba wa kijana huyo ambaye anaishi Bagamoyo mkoani Pwani.
Mpangile alisema kwa mujibu wa Baharia, baba wa kijana huyo
anayejulikana kwa jina la Akida, amesikia habari za mtoto wake na kwamba
atakwenda kuripoti kituo cha polisi.
Naye mama mdogo wa Adamu, aliyetambulika kwa jina la Khadija Katundu, alikiri maofisa wa polisi kumuhoji mume wake.
Alisema wameendelea kutoa ushirikiano kwa watu wanaofika nyumbani kwao kuhoji kuhusu suala hilo, na kwamba wanaamini ufumbuzi utapatikana.
Inasemekana kijana huyo aliwekwa rehani kwa ghamara ya Dola za Marekani 700, 000, sawa na zaidi ya Sh bilioni 1.5 za Tanzania.